
Dar es Salaam. Tundu Lissu, amewasilisha malalamiko mahakamani kuhusu wageni wake kuondolewa nchini.
Malalamiko hayo ameyawasilisha leo Oktoba 15, 2025 Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, wakati kesi ya uhaini dhidi yake ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.
Wageni hao ni Dk Brinkel Stefanie, raia wa Ujerumani na Catherine Janel Almquist Kinokfu, raia wa Marekani.
Taarifa ya Idara ya Uhamiaji iliyotolewa jana Jumanne Oktoba 14, 2025 na kusainiwa na Msemaji wake, Paul Mselle ilieleza hatua ya kuwaondosha nchini raia hao wa kigeni imechukuliwa baada ya kubainika kuwa walikiuka masharti ya viza zao za matembezi, kinyume na taratibu zilizowekwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 pamoja na Kanuni zake.
Hata hivyo, leo kabla ya kuendelea kwa kesi, Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliieleza mahakama kuwa wageni wake wameondolewa nchini kwa amri ya Idara ya Uhamiaji.
“Kabla ya kuendelea na kesi hii na mimi nina ombi juu ya haya, nimekuwa nikizungumzia hili mara kwa mara kila ninapohudhuria kesi hii na nimeacha kuzungumzia jambo hili kama mara mbili hivi,” amesema Lissu huku akipanga nyaraka zake ndani ya kizimba.
Amedai tangu kuanza kwa kesi hiyo amekuwa akiieleza mahakama jinsi ambavyo watu wamezuiwa kuingia katika mahakama hiyo na juzi hakuzungumza maana alipatiwa taarifa kwamba wangepatiwa ruhusa ya kuingia ndani ya mahakama hiyo.
Amesema taarifa alizopata ni kwamba hawakuruhusiwa na walikuja hadi lango la Mahakama Kuu na walizuiwa. Naibu Msajali wa Mahakama Kuu, Living Lyakinana aliahidi kuwa angekuwepo awasaidie.
Amesema walichukuliwa na maofisa wa Uhamiaji wakapelekwa kwenye Ofisi ya Uhamiaji na baadaye wakafuzwa nchini ili wasiweze kuingia kusikiliza kesi.
“Hii ni mara ya tatu, watu wanaotoka nje ya nchi kuja nchini kuhudhuria kesi hii wanafukuzwa na hii ilianzia kwa wale wa Kenya pale Mahakama ya Kisutu waliingia na sasa hili limetokea kwa raia wa Ujerumani na Marekani ambao wamekuja nchini kwa ajili ya kuudhuria kesi hii,” amedai Lissu na kuongeza:
“Hii ni kesi kubwa kuliko kesi zote ambayo imevuta hisia ya kimataifa na hao waliozuiliwa majina yao yapo kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na yapo katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika, hivyo siyo mambo madogo. Mahakama inapoingiliwa kwenye utaratibu wake namna hii hili siyo jambo dogo.”
Amedai mwaka 1958 kulikuwa na kesi kubwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kivukoni ambayo ilihusu Regina dhidi ya Nyerere na wenzake wawili ambayo ilikuwa ni kesi ya uchochezi ila wakoloni hawajawahi kuzuia watu na Mwalimu alitetewa na wakili kutoka Uingereza, na wakoloni hawakupeleka watu mahakamani kupiga wanaotaka kusikiliza kesi.
“Pia mwaka 1959 kulikuwa na kesi maarufu ya uhaini kule Afrika Kusini na dola ya wakati huo ilikuwa ya kikatili kwelikweli, lakini hakuna mtu aliyezuiliwa kwenda mahakamani wala aliyepigwa kwa ajili ya kwenda kusikiliza kesi,” amedai.
Lissu amedai: “Sasa nchi baada ya miaka 64 ya Uhuru, Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinatesa watu kwa kuwapiga na kuzuia wasiingie mahakamani na wanafanya mambo ya hovyo, kuliko wakoloni waliotutawala na hata kuliko makaburu waliotesa wenzetu.”
Amedai yeye yupo gerezani na hana uwezo wa kufanya chochote na mahakama imeshindwa kufanya chochote kuhakikisha watu wanaruhusiwa kuingia mahakamani.
Ameeleza yeye hawezi kingine zaidi ya kuongea ili asije kuambiwa watu wamekaa kimya pale ambapo yeye pamoja majaji wanakuwa wameshatangulia mbele ya haki.
Baada ya kueleza hayo, kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Dustan Ndunguru alimuuliza Lissu iwapo yupo tayari kuendelea kumuhoji shahidi wa Jamhuri.
Lissu alisema yupo tayari kuendelea, hivyo Jaji Ndunguru alimuelekeza amuulize maswali shahidi.