Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Omari Mwanga ‘Marioo’ amewajia juu wanaoingilia penzi lake na mama wa mtoto wake, Paula na kutoa onyo kali kwa wanaomsumbua na kutaka uhusiano wao uvunjike.
Si kazi rahisi kulinda uhusiano. Iwe ni wa marafiki au wapenzi na kinachomfanya Marioo ajiamini kwa mpenzi wake huyo ni hawezi kumsaliti na watadumu milele hadi kifo kiwatenganishe na wale wanaomvizia, watasubiri sana.
Mwananchi imemtafuta msanii huyo anayetamba na nyimbo kama Inatosha, Dear Ex, Mama Amina, Hakuna Matata, Tete, Beer Tamu, Naogopa, Dunia na nyingine nyingi ili kufunguka machache kuhusu uhusiano wake huo na juu ya yanayosemwa juu yao.
Utakumbuka uhusiano huu umekuwa ukitrendi sana na ulianza baada ya Paula ambaye ni mtoto wa mtayarishaji maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Pfunky Majani na Kajala, kubeba ujauzito wa Marioo.

Sasa juzi Jumatatu, Octoba 13, 2025 katika akaunti yake ya Instagram, Marioo amefunguka uhusiano wake na Paula umekuwa ukipigwa mawe na wengi wakisema hawatafika mbali na wapo ambao walifikia hatua ya kumshawishi Paula kutoa ujauzito alioupata.
“Nimeamua kuweka wazi unafki wote wa watu ambao wanamwambia mama mtoto wangu Paula, sababu nimeona imekuwa inazidi sasa siku hadi siku na mambo mengine yanajirudia ambayo pindi tunaanza mahusiano yalishawahi kutokea mimi nikayapotezea na kukaa kwangu kimya naona ndiyo wanazidi kupata nafasi ya kutaka kutuvuruga, ila niwaambie tu mimi na Paula tutakuwa pamoja na tutakwenda mguu kwa mguu hadi peponi, hivyo wasijiangaishe kuleta umbea umbea na unafki kwetu kwa kutaka tuachane.”

Amtofautisha Paula na wengine
“Sitaki kumaanisha niwaponde wanawake niliowahi kuwa nao, lakini kwa kweli Paula ni mwanamke wa kipekee sana kwangu. Ni mtu ambaye anajituma sana. Robo tatu ya maisha yake ni mwanamke anayefanya kazi sana, muda mwingi anafikiria maisha na ni mwanamke muelewa na mwenye upendo, amenifanya pia nimesahau hata kama nishawahi kudate na wanawake wengine najiona nimekuwa mpya tena yupo tofauti sana na wanawake wengine, hakika anajielewa.”
Wanaosema Paula ni mkorofi na jeuri, msikieni Marioo.
“Ni lazima au ni rahisi mtu kusema hivyo kwa sababu hakai naye hata kidogo na wengine hawamjui kabisa, lakini ukweli, ni mwanamke ambaye hapendi hata kidogo mambo ya ugomvi.”

Idadi ya watoto anaowataka
“Mimi napenda sana watoto na yeye anajua hilo, hivyo ni kuzidi kuomba Mungu tupate watoto wengi zaidi.”

Ugomvi kisa simu
“Hakuna kabisa na sisi kila mmoja anashika simu ya mwenzake muda wowote anaotaka, anajua namba yangu ya siri na mimi ninajua yake, ndiyo maisha yetu.”
Unamwambia nini Paula
“Nataka kumwambia nampenda sana na nitaendelea kumpenda hadi siku ninapelekwa kaburini.”
Wanafiki mpo?
“Niseme tu na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimsumbua mwanamke wangu kwa kumtongoza nawajua na wale wanawake wanaomshawishi tuachane na unafiki mwingine wote naona meseji zao zote zinazoingia katika simu ya mpenzi wangu, nawajua watu wote ambao wamekuwa wakinifanyia majungu kwa Paula, hivyo nawasubiri kuwaumbua na wala siogopi kufanya hivyo.”