Mfuko wa Mitaji ya Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wa maendeleo umefanya mkutano jijini Dar es Salaam kujadili mabadiliko ya mazingira ya ufadhili na uwekezaji katika miradi ya maendeleo, pamoja na hatua za kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa 2050.

“Huu ni wakati wa kuchukua hatua kwa pamoja na kuendana na dira ya maendeleo ya Tanzania ya 2050. Kupitia mifumo mipya ya ufadhili wa maendeleo kama vile matumizi ya raslimali za ndani, ushirikishwaji wa sekta binafsi, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, na matumizi ya hati fungani za kijani na za manispaa, tunaweza kuleta maendeleo jumuishi na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi” amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda.

Kaganda amesema dunia inatumia zaidi ya dola trilioni 2.7 kwa masuala ya usalama, kiasi ambacho kingetosha kumaliza njaa na kuboresha huduma za afya duniani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa, Dkt. Fred Msemwa amesema dira ya 2050 inalenga kuweka sekta binafsi kama injini kuu ya uchumi huku serikali ikibaki kuwa mwezeshaji na mpunguzaji wa hatari kwa wawekezaji.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Susan Nyamondo amesema maarifa yaliyopatikana katika mkutano huo yatasaidia kuoanisha vipaumbele vya serikali na washirika wa maendeleo, akitolea mfano hati fungani ya kijani ya Tanga UWASA kama ubunifu wa ufadhili unaoweza kuigwa.

Wadau wengine akiwemo John Viner kutoka Ubalozi wa Sweden na Samwel Kilua wa Gatsby Africa wamesisitiza umuhimu wa kuongeza ushirikiano na matumizi bora ya rasilimali. Wamewahimiza wadau kuendeleza ubunifu, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi, na kupanua miradi iliyofanikiwa ili kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu kuelekea dira ya 2050.

#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *