Umoja wa Ulaya unakabiliwa na idadi kubwa ya watu wasio na makazi inayoongezeka kwa kasi, mzozo ambao unachukua sura mpya kila siku.
Shirikisho la Mashirika ya Kitaifa ya Wasio na Makazi (Feantsa) limetangaza katika ripoti yake mpya kwamba, idadi ya watu wasio na makazi katika Umoja wa Ulaya inaongezeka kwa kasi ya kutisha.
Ripoti hiyo inakuja huku Umoja wa Ulaya ukidai kuwa, unafanyia kazi lengo lake kubwa la kumaliza ukosefu wa makazi ifikapo mwaka 2030, lengo ambalo kwa mwendo wa sasa linaonekana kuwa mbali kufikiwa.
Chimbuko la mgogoro huu lazima ichunguzwe katika hali mbaya ya kiuchumi na kupungua kwa uwezo wa kifedha wa serikali za Ulaya na wananchi. Kupanda mfumuko wa bei, kuongezeka viwango vya riba, kudumaa uzalishaji, na kushuka uwezo wa kununua kumezifanya familia nyingi kuwa kwenye ukingo wa kuporomoka kifedha.
Kwa upande mwingine, matokeo ya moja kwa moja ya vita vya Ukraine na sera za gharama kubwa za kuunga mkono Kiev zimekuwa na mashinikizo makubwa katika bajeti za umma za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Mabilioni ya Euro ambayo yangeweza kutumika katika kujenga makazi ya kijamii, kuimarisha msaada wa ustawi na kupunguza mfumuko wa bei sasa yanatumika kutuma silaha, nishati na misaada ya kifedha kwenye uwanja wa vita.

Kusitishwa uagizaji wa nishati ya bei nafuu kutoka Russia nako kumetoa pigo maradufu dhidi ya uchumi wa Ulaya. Kupanda kwa bei ya nishati kumezifanya gharama ya maisha kufikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa, na kusababisha bei ya nyumba na kodi kupanda juu.
Benki Kuu ya Ulaya imeongeza viwango vya riba katika jaribio la kukabiliana na mfumuko wa bei, lakini uamuzi huo umefubaza soko la ujenzi na kufanya mamilioni ya Wazungu kushindwa kumudu mikopo ya nyumba.
Kwa utaratibu huo, mzunguko umeundwa ambapo sera za uchumi mkuu zenyewe zimekuwa injini ya ukosefu wa makazi.
Mbali na hayo, mabadiliko ya kisiasa kuelekea vyama vya mrengo wa kulia na kupunguzwa bajeti za kijamii katika baadhi ya nchi za Ulaya kumeifanya hali kuwa mbaya zaidi. Sio tu kwamba sera mpya hazijasaidia kuboresha hali ya makazi, lakini kwa kuziwekea vikwazo asasi za kiraia (NGOs) na kupunguza usaidizi kwa makundi yaliyo hatarini, zimefungua njia ya kuenea umaskini mijini na ukosefu wa makazi zaidi.
Mazingira haya yameifanya Ulaya leo kukabiliwa na ukweli mchungu wa mgawanyiko mkubwa wa matabaka, kushadidi mfumuko wa bei, uzalishaji uliodumaa, na wimbi jipya la ukosefu wa makazi katikati ya miji ambayo wakati fulani ilikuwa nembo ya ustawi wa kimataifa na mfumo wa kiuchumi.
Kwa mtazamo mwingine, mgogoro wa ukosefu wa makazi unaweza kuonekana kama tatizo la kijamii tu, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, hii ni ishara ya wazi ya mgogoro wa kina katika muundo wa kiuchumi na usimamizi wa Ulaya.
Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, karibu watu milioni mbili hawana makazi katika nchi mbalimbali za Ulaya. Nchini Ujerumani, nchi ambayo ni kinara wa nguvu za kiuchumi barani Ulaya, zaidi ya watu nusu milioni hawana makazi. Katika Jamhuri ya Ucheki, nchi yenye wakazi milioni kumi tu, zaidi ya watu 230,000 hawana makazi. Hata nchi zinazoongoza katika ustawi wa jamii kama vile Finland, Denmark na Ireland zimo katika mkongo wa kuongezeka katika janga hili.

Katika miji mikuu kama vile Berlin, Paris, Amsterdam na Dublin, bei za kukodisha nyumba zimeongezeka sana na kutenga sehemu kubwa ya tabaka la wafanyakazi na hata tabaka la kati, na kubadilisha umiliki wa nyumba barani Ulaya kutoka katika hali ya haki ya kijamii hadi ndoto isiyoweza kutimia.
Tofauti hii kati ya malengo ya Umoja wa Ulaya na uhalisia wa maisha ya raia wake imetilia shaka sana uhalali wa muundo wa kisiasa wa umoja huu.
Nchini Finland, nchi ambayo wakati mmoja ilisifika kwa kukomesha ukosefu wa makazi, filihali mitaa yake imejaa tena watu walioathiriwa na msukosuko wa kisiasa na kupungua uungaji mkono wa kijamii. Huko Hungary, serikali ya Waziri Mkuu Viktor Orban imeshinikiza mashirika ya kiraia, na kufikia hatua ya kuzuia uchapishaji wa takwimu halisi za ukosefu wa makazi.
Ulaya leo si bara la mshikamano wa kijamii tena; bali ni mkusanyiko wa serikali zenye wasiwasi wa mustakabali, zilizonasa katika kinamasi cha ushabiki wa ndani na sera za kigeni za gharama kubwa.
Uhalisia wa mambo ni kuwa, ukosefu wa makazi barani Ulaya, ni kioo ambacho sura ya kweli ya mgogoro wa ustaarabu wa Magharibi inaonekana. Bara tajiri lenye watu wasioweza kujipatia mahitaji yao ya kimsingi, yaani nyumba ya kuweza kujistiri.
Katika uwanja huo, ikiwa viongozi wa Ulaya wataendelea kufuata vipaumbele vyao vibaya, historia inaweza kukumbuka miaka ya 2020 sio kama kipindi cha kutetea demokrasia nchini Ukraine, lakini kama mwanzo wa kuzorota kwa ustawi wa jamii huko Ulaya.