Marekani. Baada ya kupitia moja ya kesi kubwa zaidi katika maisha yake, mwaka 2005 marehemu staa wa muziki duniani Michael Jackson aliamua kuondoka kabisa Marekani na kuelekea Bahrain, taifa dogo lililoko Ghuba ya Uajemi.
Kutokana na kesi hiyo inaelezwa msanii huyo alichukua uamuzi wa kuvaa Abaya pamoja na Nikabu ili kuepuka mashabiki na paparazi waliokuwa wakimuandama. Kesi hiyo ni ile iliyomuhusisha kijana mmoja aliyedai MJ alimnyanyasa kingono akiwa katika makazi yake huko Neverland Ranch.

Kwa miezi kadhaa, mashahidi mbalimbali walitoa ushahidi huku vyombo vya habari vikimfuatilia msanii huyo kila hatua. Lakini Juni 2005, majaji walimkuta hana hatia katika mashitaka yote na kufutiwa kabisa mashtaka hayo.
Aidha baada ya kuumizwa na kitendo hicho watu wa karibu wa MJ wanaeleza msanii huyo alikata tamaa ya kuishi Marekani ndipo akaamua kupokea mwaliko wa muda mrefu kutoka kwa Sheikh Abdulla bin Hamad Al-Khalifa, mwana wa mfalme wa Bahrain, ambaye alikuwa shabiki yake mkubwa.
Mwanamfalme huyo alimpa hifadhi, nyumba ya kifahari na faragha msanii huyo aliamua kuishi maisha yake huku mara nyingi akionekana anatembelea maduka makubwa akiwa amevalia Abaya na Nikabu ili kuficha uso wake.
Vazi hilo kwa kawaida ni marufuku kuvaliwa na wanaume katika nchi za Kiarabu, lakini kwa sababu alikuwa chini ya ulinzi wa kifalme, hakukamatwa wala kuhojiwa.
MJ aliishi Bahrain takribani mwaka mmoja ambapo alihamia katika mji huo mwishoni mwa mwaka 2005 na kuishi chini ya ulinzi wa kifahme hadi mwishoni mwa mwaka 2006.

Hata hivyo, kufikia mwanzoni mwa mwaka 2007, uhusiano wake na Sheikh Abdulla ulianza kuyumba kutokana na tofauti za kifedha na miradi ya muziki ambayo haikufanikiwa, ambapo MJ alichukua uamuzi wa kuhamia Ireland ambapo aliendeleza maisha yake.
Utakumbuka Michael Jackson alifariki dunia Juni 25, 2009, akiwa na umri wa miaka 50. Huku sababu ya kifo chake ikitajwa kuwa ni overdose ya dawa za usingizi aina ya propofol, ambayo ilipelekea moyo wake kusimama ghafla.