
ALIKUWA akilitazama gereza hilo kama vile ndio ilikuwa mara yake ya kwanza alikuwa akiliona.
Baada ya kutafakari kwa muda alikumbuka kile kilichokuwa kikimfanya awe katika hali hiyo, kwanza alianza kukumbuka kilichomfanya afikie hatua ya kuingizwa gerezani, kisha ndipo kumbukunmbu ya kile alichokutana nacho ndani ya gereza hilo zilirejea tena akilini mwake.
Matukio kadhaa yaliyojiri yalijirudia na kama haitoshi alikumbuka mkasa mzima uliomfanya ahukumiwe kifungo na kupoteza haki na uhuru wake wa kuishi uraiani.
Hapo ndipo alipokumbuka hatua kubwa za kimaisha alizokuwa amezipiga katika kutimiza ndoto zake za kimaendeleo. Ndoto ambazo zilikuwa tayari zimeshafanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini zikafutika ghafla kama donge la samli katika kikaango cha moto kutokana na makosa aliyoyafanya.
Kumbukumbu hiyo mbaya ilimfanya kutikisa kichwa kuonyesha ishara ya kuyajutia yaliyomsibu.
Ghafla kama mtu aliyezinduliwa kutoka katika usingizi mzito, aligeuka na kutazama mbele kisha akapiga hatua za taratibu kuendelea na safari yake akiliacha eneo la magereza.
Alikuwa akitembea kwa mwendo wa kawaida kutokana na unyonge uliokuwa umemtawala baada ya kuukumbuka mkasa uliomfanya ahukumiwe kifungo.
Akiwa ameshika njia ya kuelekea kituoni kutafuta usafiri wa kumfikisha maeneo aliyokuwa akiishi na kuonana na ndugu na jamaa zake kwa mara nyingine, akakumbuka kitu kingine cha muhimu zaidi alichokutana nacho ndani ya gereza hilo.
Pamoja na uchungu wote aliokuwa nao alijikuta akiachia tabasamu la matumaini. Halikuwa tabasamu halisi lililotoka chini ya uvungu wa moyo wake, bali lilikuwa ni lile tabasamu la kulazimisha kwa kuwa hakuwa na uhakika na ahadi aliyokuwa amepewa kama ingeweza kutimia.
Pamoja na kutokuwa na uhakika na ahadi hiyo, taratibu moyo wake ulianza kupata faraja na kurejewa na amani.
Ahadi aliyopewa ilimfanya kurudisha matumaini ya maisha yake ya baadaye.
***
KAMBA Makambo mfanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hakuyaamini macho yake na alibaki akiwa amepigwa na butwaa kwa kile kilichokuwa kimetomkea.
Kamba alipigwa na butwaa na kutahayari. Ni baada ya kutoliona gari alilokuwa amelikodi kwa ajili ya kununua bidhaa katika maduka yalioko katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika kutaka kuhakikisha, aligeuka kila upande huku akiangaza kwa umakini akiamini labda angeweza kuliona gari hilo au hata kumuona dereva wa gari hilo, lakini hakuambulia kitu.
Bado hakutaka kuamini kama alikuwa ameibiwa. Hakutaka kujipa presha kwa kitu cha kusadikika, aliendelea kuvuta subira akiamini angeweza kuliona gari hilo kwa mara nyingine.
Lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo Kamba alivyoanza kuingiwa na wasiwasi kutokana na kutoyaona matarajio yake.
Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, akili yake ilianza kuvurugika na kushindwa kufanya kazi sawasawa. Raia huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aligeuka na kuwa kama mtu aliyekuwa akikaribia kuchanganyikiwa kama sio kupatwa na ugonjwa wa wazimu.
Takribani dakika kumi na tano zilizozopita, Kamba alikuwa amemuacha dereva wa teksi aliyemkodi kutoka hotelini alikofikia nje ya duka akitafuta nafasi ya kuegesha gari hilo.
Kamba hakuwa na wasiwasi kwasababu kulikuwa na nafasi kubwa ya kuliegesha gari hilo nje ya duka alilokuwa amedhamiria kuingia kununua bidhaa.
Wakati Kamba alipokuwa akiingia katika duka hilo ili kuendelea kufanya manunuzi ya bidhaa alizokuwa akizihitaji, ni wakati huo ambao dereva wake alikuwa akihangaika kuliegesha gari hilo nje ya duka alilokusudia kuingia.
Kamba hakutaka kumwangalia dereva hadi mwisho kama aliiigesha gari lile pale au la… kwa haraka aliingia ndani ya duka alilokuwa amelikusudia.
Mara baada ya kumaliza kufanya manunuzi na kurudi eneo alilomuacha dereva, ndipo Kamba alipogundua kutokuwepo kwa gari hilo na kuanza kuingiwa na wasiwasi.
Kwanza hakutaka kuamini moja kwa moja kama dereva aliyekuwa naye alikuwa amemtoroka, aligeuka huku na kule, kisha alipiga hatua kadhaa kuufuata Mtaa wa Congo lakini hakuwa na matumaini ya kuliona gari mbele yake, hadi kufikia hatua hii Kamba alianza kuingiwa na shaka kwani kila alivyopiga hatua ndivyo alivyozidi kuchanganyikiwa zaidi.
Hata hivyo, akili ya Kamba ilikuwa inagoma kukubaliana na ukweli kama dereva aliyekuwa ameambatana naye kufanya naye manunuzi ya bidhaa alikuwa amemtoroka.
Kamba iliingiwa na matumaini hayo kutokana na imani yake kwa Watanzania, aliwaamini kutokana na ukarimu na uaminifu wao, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukisonga ndivyo imani na matumaini yake yalivyokuwa yakitoweka katika nafsi yake.
Taratibu matumaini yakaanza kupotea na kuanza kuzungumza peke yake kama mtu aliyechanganyikiwa. Maneno yaliyokuwa yakimtoka kinywani mwake hayakusikika na watu wengine aliokuwa akipishana nao na hata wale waliokuwa wakiendelea na shughuli zao katika kitongoji hicho chenye pilikapilka nyingi.
Akiwa amezishika au amezikumbatia bidhaa alizokuwa ametoka kuzinunua, matumaini ya kuliona gari au dereva wa gari hilo yalishatoweka akilini mwake. Hatimaye alikata shauri kurudi nyuma hadi usawa wa duka alilofanya manunuzi lakini bado hakuacha kuangaza huku na kule akihisi labda angeweza kuliona gari alilokuwa amerikodi ama dereva wake.
Lakini matumaini ya kuliona gari yalitoweka, akiamini kulikuwa na uwezekano wa kuzidiwa maarifa na dereva aliyekuwa amemkodi.
Hali ilivyozidi kuwa mbaya na matumaini ya kuliona gari yalivyokuwa yakizidi kutoweka, Kamba alifikia hatua ya kulitafuta gari kwenye mifuko yake ya suruali.
Tukio la kuibiwa lilimfanya achanganyikiwe mara mbili, kwanza ni kutokana na hofu ya kuibiwa na pili ni joto la Dar es Salaaam ambalo wakati huo ndio lilikuwa limeshika kasi kwelikweli.
Kamba alikuwa akilisikia joto hilo lililokuwa likifukuta hadi ndani ya mwilini mwake.
Siku zote Kamba hakuweza kulistahamili joto la Dar es Salaam, alihisi kama vile alikuwa akiadhibiwa kutokana na mwili wake mkubwa kumchomachoma na kumsababishia mateso kiasi cha kutamani kuzivua nguo alizokuwa amezivaa.
Fukuto la kuibiwa lilikuwa likiuchoma na kuumiza moyo na akili yake wakati joto lilikuwa likiuadhibu mwili wake na kumfanya kuwa kwenye mateso makubwa.
Kamba alitoa kitambaa na kujifuta kujaribu kupunguza kasi ya jasho lililokuwa likimchuruzika kwenye paji lake.
Kitu kingine kikaibuka na kuikera akili yake, ni kama vile ndio kwanza alikuwa akikisikia. Zilikuwa ni kelele za Wamachinga waliokuwa wameizunguka mitaa ya Kariakoo.
Wamachinga ambao hutumia spika na midomo yao kunadi biashara zao kwa wapita njia.
Kutokana na kuvurugwa kwa kuibiwa na joto la Dar es Salaam, kelele hizo zilimtesa Kamba na kumfanya azidi kuchanganyikiwa. Alihisi kama vile zilikuwa zikipigwa kutokea kichwani mwake.
Raia huyo wa Demokrasia ya Congo alitamani kuwa na mamlaka ya kuwanyamazisha Wamachinga wale mara moja lakini hakuwa na ubavu wa kufanya hivyo.
Kamba akazidi kuvurugwa.
***
MARA kwa mara Kamba amekuwa akifanya safari zake Tanzania, hususan katika Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kununua bidhaa na kwenda kuziuza nyumbani kwao katika Jiji la Lubumbashi.
Katika jiji hilo la pili kwa ukubwa katika nchi ya Congo DR, Kamba alikuwa ni mmoja kati ya wafanyabiashara wanaoheshimika kutokana na bidhaa zake alizokuwa akizinunua Tanzania.
Safari hii kama zilivyokuwa nyingine, alikuwa katika jiji hilo kwa ajili ya kununua bidhaa katika maduka ya jumla na katika baadhi ya viwanda vinavyopatikana katika jiji hilo.
Kamba alikuwa amefikia katika Hoteli ya Lambodin iliyopo Sinza Afrika Sana. Akiwa hotelini hapo, alichoka kumsubiri dereva wake wa siku zote aliyekuwa akimchukua na kumuongoza kwenda kununua bidhaa katika maduka mbalimbali.
Akiwa amefikia katika hoteli hiyo kwa ajili ya biashara zake, usiku wa siku moja kabla ya tukio, Kamba alimpigia simu dereva wake kumkumbusha kuhusu safari yao ya kwenda kununua bidhaa kama ilivyokuwa desturi yao.
Kama haitoshi asubuhi na mapema ya siku husika, Kamba kwa mara nyingine tena, alimpigia simu dereva wake na kumkumbusha kuhusu ahadi ya kuwahi kufika hotelini.
Dereva alimhakikishia angeweza kuwahi na kufanikisha jambo hilo kama ilivyokuwa kawaida yao.
Muda walioahidiana ulipokuwa ukikaribia, Kamba kwa mara nyingine tena alimpigia dereva wake ambaye naye alimhakikishia kuwa alikuwa njiani kufika hotelini.
Akiwa na matumaini ya kuwahi katika pilikapilika zake, Kamba alishuka kutoka ghorofa ya tatu ya hoteli hiyo na kumsubiri dereva kwasababu alikuwa ameshajindaa tangu mapema.
Lakini baada ya kushuka na kusimama karibu na sehemu ya maegesho ya magari ya hoteli hiyo, kila alipopiga simu, aidha dereva hakuipokea au alipoipokea aliendelea kumjibu kuwa hakuwa mbali kufika hotelini hapo.
Muda ulizidi kwenda bila ya dalili za dereva kutokea na ilifika hatua Kamba alikata tamaa baada ya kuchoka kuvumilia.
Inaendelea…