Lindi. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza Tanzania, mojawapo ya mambo ya kwanza atakayoyafanya ni kufuta mpango wa kuisafirisha gesi ghafi kutoka Lindi, na badala yake atahakikisha inachakatwa mkoani humo kabla ya kusafirishwa nje.
Mwalimu ametoa ahadi hiyo leo Jumatano Oktoba 15, 2025, katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Kata ya Mnazi Mmoja, mkoani Lindi, ikiwa ni mkutano wake wa mwisho katika mkoa huo.

Mwalimu amefanya mikutano yake katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Masasi na Lindi Mjini, akisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali mahali zinapopatikana ili ziwanufaishe wananchi wa eneo husika.
“Gesi ikichakatwa hapa Lindi, kutaanzishwa viwanda, madereva watapata ajira za kuisafirisha, migahawa itafunguliwa na watakaohudumu watakuwa ninyi wananchi wa Lindi. Hata wauzaji wa nyanya na kahawa watanufaika moja kwa moja,” amesema Mwalimu.
Amesema upatikanaji wa gesi hiyo utaongeza kipato cha wananchi kwa kuwa wakazi wa eneo hilo wataweza kuuza mitungi ya gesi nyumbani na kwenye migahawa kwa wingi zaidi.
“Kama ulikuwa unauza mitungi 10 kwa mwezi, sasa utauza 20, maana gesi itapatikana hapahapa,” amesema.
Mgombea huyo amesema utekelezaji wa mpango huo pia utachochea ujenzi wa nyumba za kulala wageni na hivyo kuongeza ajira kwa vijana wa eneo hilo.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuikosoa serikali iliyopo madarakani, akisema wananchi wanapaswa kufanya uamuzi sahihi siku ya kupiga kura kwa kukichagua Chaumma, kwa sababu Serikali ya CCM iliyodumu kwa miaka 60 madarakani, imeshindwa kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi.

“Mungu amewajalia mafuta, gesi, korosho na bidhaa adimu duniani. Dawa ni moja tu, chagueni Chaumma muone tutakavyotumia rasilimali zenu kuwaletea maendeleo,” amesema.
Mwalimu amesema haoni sababu kwa mikoa yenye bandari za asili kama Lindi, Tanga na Mtwara kuendelea kuwa maskini.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo mgombea ubunge wa Chaumma, Honoratus Daud, ameeleza changamoto za maisha zinazosababishwa na umaskini, ikiwamo kuvunjika kwa ndoa nyingi licha ya wanandoa kuendelea kupendana.
“Ndoa nyingi zinavunjika si kwa sababu ya chuki, bali umaskini. Unamwachia mke Sh5,000 ukiwa na familia ya watu sita anajitahidi kujiongeza ndipo unamfumania na kumuacha, wakati bado unampenda,” amesema Daud.
Hivyo, ameahidi endapo wananchi wa Lindi watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao, atapigania ujenzi wa viwanda 10 ndani ya miaka mitano vitakavyosaidia kuongeza ajira kwa vijana.
Amesema dunia ya sasa inaendeshwa kidijitali, chama chake kitahakikisha kila kijiji, mtaa na kijiwe kinapata mtandao wa bure (WiFi) ili vijana waweze kufanya biashara na kujifunza mtandaoni.

Katika hatua nyingine, Daud amemuomba mgombea urais (Mwalimu) akiingia madarakani, Serikali yake iurejeshe mjusi wa pekee wa Lindi ambao alipelekwa Ulaya kwa maonesho ya utalii, akisema alikuwa chanzo cha mapato kwa wananchi.
“Mjusi yule wa asili alikuwa kivutio cha kipekee kilichotuletea watalii na kipato. Tunataka arudishwe, sio huyu wa plastiki asiyeleta faida,” amesema.