Dar es Salaam. Mwanasiasa mashuhuri kinara wa upinzani na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga (80) amefariki dunia leo Jumatano ya Oktoba 15, 2025.

Odinga maarufu ‘Baba’, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Sreedhareeyam Ayurvedic, huko Kerala nchini India baada ya kupata shambulio la moyo, vyanzo mbalimbali vimeripoti.

Kwa mujibu wa tovuti ya Nation ya Kenya, Rais William Ruto na familia ya Odinga wamethibitisha taarifa hiyo.

Odinga alipatwa na mshtuko wa moyo wakati wa matembezi ya asubuhi katika hospitali hiyo ambako amekuwa akitibiwa kwa siku zote alipokuwa huko.

Taarifa zaidi zinasema alipelekwa nchini India Oktoba 3, mwaka huu kwa ajili ya uangalizi zaidi wa afya yake. Kaka yake mkubwa na Seneta wa Siaya, Oburu Oginga ambaye ndiye msemaji wa familia amesema.

Odinga amekuwa akisafiri kila mara kwa uchunguzi kufuatia upasuaji wake wa kichwa alioufanya  Juni, 2010 ili kupunguza shinikizo lililokuwa limeongezeka nje ya ubongo wake.

Historia yake

Odinga alizaliwa Januari 7, 1945 huko Maseno, Wilaya ya Kisumu. Anatoka katika familia mashuhuri ya kisiasa. Baba yake, Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya (1964–1966) na alikuwa kiongozi muhimu katika harakati za uhuru.

Odinga alisoma katika nchi za Afrika Mashariki kabla ya kwenda Ulaya kwa masomo ya juu. Alipata digrii ya uhandisi mitambo na uhandisi wa umeme kutoka Technical University of Magdeburg (zamani ilikuwa Ujerumani Mashariki) mnamo mwaka 1970.

Baada ya kurejea Kenya, alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Nairobi na baadaye katika Shirika la Viwango la Kenya (Kenya Bureau of Standards – KBS), ambapo alihudumu kama Naibu Mkurugenzi.

Alijiunga na siasa mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 akawa mmoja wa viongozi walioshinikiza kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Kenya.

Kwa sababu ya misimamo yake ya kisiasa, hasa wakati wa utawala wa Rais Daniel Moi, alifungwa mara kadhaa bila kesi, akitumia jumla ya miaka tisa gerezani.

Hadi umauti unamkuta Odinga amewahi kuwa mbunge ambapo mara ya kwanza alichaguliwa kuwa mbunge wa Lang’ata mwaka 1992.

Aliwahi kuwa Waziri wa Nishati (2001-2002) chini ya Rais Moi. Waziri wa Barabara, Ujenzi na Makazi (2003-2005): Chini ya Rais Mwai Kibaki.

Waziri Mkuu (2008-2013): Hii ilikuwa nafasi aliyoshikilia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi wa mwaka 2007.

Katika kiti cha urais Odinga amegombea urais wa Kenya mara tano bila kufanikiwa kushinda kiti hicho.

Miongoni mwa matukio katika historia yake ni lile la “Handshake” (Mwafaka): Tukio muhimu katika historia yake ya hivi karibuni ni mwafaka na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2018, ambao ulimaliza mzozo mkubwa wa kisiasa na kuleta utulivu.

Anatajwa sana kama “Baba” au kiongozi wa upinzani nchini Kenya, akisimamia chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na vyama vingine vya mrengo wa upinzani. Alikuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya na za Afrika.

Odinda pia aliwahi kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mwaka huu ambapo hakufanikiwa kuipata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *