Nairobi – Kenya imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani na mwanasiasa mashuhuri, Raila Amolo Odinga, ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Raila alifariki kutokana na mshtuko wa moyo akiwa anapokea matibabu katika Hospitali ya Kochi nchini India
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kifo chake kimezua maombolezo makubwa nchini Kenya na katika mataifa mbalimbali ya Afrika, ambako aliheshimika kama kiongozi mwenye maono na msimamo thabiti.
Katika historia ya siasa za Kenya, Raila Odinga ameacha alama isiyofutika. Akiwa kiongozi wa chama cha ODM na mshiriki mkuu katika harakati za kurejesha mfumo wa vyama vingi, alichangia pakubwa katika mageuzi ya katiba, haki za kiraia, na mapambano dhidi ya ufisadi. Ingawa hakuwahi kufanikisha azma yake ya kuwa Rais, Raila alibaki kuwa sauti ya matumaini kwa wengi waliotamani mabadiliko ya kweli katika uongozi wa taifa.

Mchango wa Raila haukuishia ndani ya mipaka ya Kenya pekee. Alikuwa kiungo muhimu katika juhudi za kutafuta amani na maridhiano katika kanda ya Afrika Mashariki na bara zima. Aliteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mjumbe wa maendeleo ya miundombinu barani Afrika, jukumu ambalo alilitumia kuhimiza ushirikiano wa kieneo na maendeleo jumuishi. Uwepo wake katika majukwaa ya kimataifa uliifanya Kenya kujulikana zaidi kama taifa lililo mstari wa mbele katika siasa na maendeleo ya Afrika.
Kifo cha Raila Odinga kinawakilisha mwisho wa enzi ya mwanasiasa aliyewakilisha matumaini, uthubutu, na mapambano ya kidemokrasia. Taifa la Kenya linaomboleza, bara la Afrika linakumbuka, na historia itamhifadhi kama mmoja wa viongozi waliotia alama ya kudumu katika siasa za kizazi hiki. Ratiba ya mazishi na shughuli za kitaifa za maombolezo zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Hivi karibuni alifanikisha umoja wa kitaifa kwa kujiunga na Rais aliyeko madarakani William Ruto baada ya kushuhudia wimbi la machafuko ya kisiasa hatua ambayo imeshuhudia utulivu wa kitaifa