
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Raila Odinga alikuwa mmoja wa watu mashuhuri wa kisiasa nchini Kenya licha ya kuwania urais mara tano bila mafanikio.
Kwa miaka kadhaa, mwanasiasa huyo mkongwe aliibuka kuwa kiongozi shupavu na mtetezi wa demokrasia ya vyama vingi – aliye enziwa sana na wafuasi wake na kushutumiwa vikali na wapinzani wake wa kisiasa.
Kiongozi huyo mkongwe wa upinzani alifariki dunia Jumatano asubuhi akiwa na umri wa miaka 80 nchini India, ambako alikuwa akipokea matibabu kutokana na ugonjwa ambao haukujulikana.
Kifo chake sio tu kinaashiria mwisho wa enzi ya mwanamageuzi wa Kiafrika, lakini pia kinaacha pengo kubwa katika upinzani wa Kenya wakati nchi hiyo inaelekea uchaguzi wa 2027.
Ingawa Odinga alitoka katika familia maarufu ya Kenya, taji la kisiasa lilimponyoka katika kipindi chote cha maisha yake ya miongo kadhaa – kama vile lilivyomkwepa babake, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais baada ya Kenya kupata uhuru wake kutoka Uingereza.
Mnamo 2022, Odinga aliwania kwa mara tano kiti cha urais, baada ya kukaribia wadhifa huo wa juu mwaka wa 2008 alipoteuliwa kuwa waziri mkuu katika serikali ya mseto ya Hayati Rais Mwai Kibaki.
Mwezi Februari, alishindwa na waziri wa mambo ya nje wa Djibouti katika kinyang’anyiro cha Uwenye Kiti wa Kamisheni ya Tume ya Umoja wa Afrika.
Licha ya masaibu yake ya kisiasa, Odinga alisalia kuwa kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa hivi kwamba marais waliofuata wa Kenya walitatizika kuongoza kwa urahisi bila uungwaji mkono wake.
Mwaka jana, Rais William Ruto aliwasiliana na Odinga kwa makubaliano ya kisiasa ambayo yalishuhudia viongozi wa upinzani wakiteuliwa katika baraza la mawaziri.
Wanachama wanne wa chama cha ODM cha Odinga walijiunga na serikali ambayo sasa inajulikana kama “Broadbase”.
Hatua hiyo ilionekana na wengi kama jaribio la Ruto kuimarisha mamlaka yake kufuatia ongezeko la hali ya manung’uniko miongoni mwa Wakenya dhdi ya utawala wake kwa kushindwa kuboresha maisha ya watu maskini, huku akipandisha kodi kwa kiwango cha juu.
Odinga alikabiliwa na ukosoaji mkubwa, kutoka kwa vijana maarufu Gen Z ambao waliongoza maandamano ya kupinga serikali. Vijana hao walimshutumu kwa kuhujumu juhudi zao za kupigania utawala bora. Raila hata hivyo alisisitiza kuwa “alitoa” ushauri wa kitaalamu tu kumsaidia rais “kuokoa” nchi.
Raila ambaye alikuwa shabiki mkubwa wa klabu ya Ligi kuu ya England ya Arsenal, anatokea jamii ya Waluo – ya nne kwa ukubwa nchini Kenya.
Alikuwa na ufuasi mkubwa wa kisiasa na wanachama wake walimpatia majina tofauti ya utani kama vile “Agwambo” na”Tinga” – majina ambayo yalitokana na inembo ya chama chake katika uchaguzi wa mwaka1997.
Mtindo wake wa kucheza densi kwa upole hasa muziki wa reggae katika mikutano yake ya kisiasa – ulipata umaarufu hadi ikaitwa “Densi ya Raila” – na kuigwa na wengi katika mikusanyiko ya kijamii.
Katika uchaguzi wa urais wa 2022, Odinga alimchagua aliyekuwa Waziri wa Sheria Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake. Hatua hiyo ilipongezwa sana, kwani ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mgombeaji urais kumchagua mwanamke kama mgombea mwenza.
Odinga alionekana kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake, Jaramogi Odinga, ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya baada ya uhuru, lakini akajiondoa serikalini mwaka 1966 baada ya kutofautiana na kiongozi wa wakati huo Jomo Kenyatta, ambaye mtoto wake, Uhuru, aliishia kuwa rais baada ya ujio wa demokrasia ya vyama vingi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Jaramogi Odinga alivutiwa sana siasa za Umoja wa Kisovieti na China, huku Jomo Kenyatta akipendelea muungano na Marekani na mataifa mengine yenye nguvu za Magharibi.
Tofauti zao zilizidi kuwa mbaya, ambapo Jaramogi Odinga alifungwa kwa miezi 18 hadi alipoachiliwa mnamo 1971.
Raila Odinga pia alikuwa mfungwa wa zamani wa kisiasa, na anashikilia rekodi ya kuwa mfungwa aliyetumikia kifungo cha muda mrefu zaidi nchini Kenya.
Mapambano yake dhidi ya utawala wa chama kimoja yalimfanya azuiliwe mara mbili (kutoka 1982 hadi 1988 na 1989 hadi 1991) wakati wa utawala wa mrithi wa Jomo Kenyatta, Daniel arap Moi.
Awali alifungwa gerezani kwa kujaribu kufanya mapinduzi mwaka 1982, ambayo yalimweka kwenye ramani ya kitaifa.
Baada ya demokrasia ya siasa za vyama vingi kuanzishwa muongo mmoja baadaye, Odinga alishindwa mara kwa mara katika jaribio lake la kuwa rais wa Kenya, mara kwa mara akidai kuwa ushindi wake uliibwa.
Hii ilisababisha mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa katika historia ya Kenya, wakati takriban watu 1,200 walipouawa na maelfu kukimbia makazi yao baada ya Odinga kushawishika kuwa Rais wa wakati huo Mwai Kibaki alichakachua uchaguzi wa 2007.