Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa anatarajiwa kuzuru Moscow Jumatano, kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Syria na chanzo cha serikali kilichonukuliwa Jumanne, licha ya kusogezwa mbele kwa mkutano wa kilele wa Kiarabu aliokuwa akitarajia kuhudhuria.
Chanzo cha serikali kimesema Sharaa atafanya mazungumzo kuhusu mustakabali wa uwepo wa vituo vya kijeshi vya Urusi – bandari ya Tartous na kituo cha anga cha Hmeimim – vilivyobaki nchini humo tangu enzi za utawala wa Bashar al-Assad.
Kuomba kumkabidhi Bashar al-Assad
Aidha, Sharaa anatarajiwa kuwasilisha ombi rasmi kwa Urusi kumkabidhi Assad, aliyepinduliwa na kupewa hifadhi ya kisiasa mjini Moscow, ili afikishwe mahakamani kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya wananchi wa Syria.
Sharaa, ambaye hapo awali aliwahi kuongoza tawi la al-Qaeda nchini Syria kabla ya kujiunga na waasi waliouteka mji wa Damascus mwezi Desemba, sasa anaendesha serikali mpya ambayo Urusi imejaribu kuendeleza uhusiano nayo kupitia diplomasia na msaada wa kijeshi kufuatia mashambulizi ya Israel nchini humo.