Mwanza. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewataka watendaji wa Serikali wanaosimamia na kutekeleza miradi ambayo inapata ufadhili wa mashirika ya kimataifa, kuhakikisha fedha zinazoainishwa katika utekelezaji huo hazitumiki vibaya na kuchepshwa, ili malengo ya miradi hiyo yatimie na kutolichafua jina la nchi.
Biteko ametoa kauli hiyo leo Oktoba 15, 2025 jijini Mwanza wakati akizindua mfuko wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko (Pandemic Fund in Tanzania), wenye lengo la kuimarisha uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya mlipuko na dharura nyingine za kiafya nchini.
Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) kwa ufadhili wa The Pandemic Fund kwa gharama ya zaidi ya Sh95 bilioni (Dola za Marekani 38.7 milioni), huku ukiifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani zitakazonufaika na mradi huo.

Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko akibonyesha kitufe kuashiria uzinduzi wa mfuko wa kukabili magonjwa ya mlipuko (Pandemic Fund in Tanzania), leo jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati amesema matarajio ya Serikali ni kuona fedha hizo ambazo zinatoka kwa wafadhili na zile zitakazotoka kwa walipa kodi wa Tanzania zinasimamiwa vizuri na kuleta matokeo chanya.
”Sekta zote zinazohusika kwenye mfuko huu zisimamie kikamilifu ili matokeo yapatikane kwa sababu imekuwa kawaida kuwa na maandiko mazuri lakini malengo yanachepushwa. Mambo tuliyoyaandika kwenye mradi utekelezaji uwe ni uleule, tuyatekeleze ili tuwape hakikisho na uaminifu wa nchi yetu katika ufadhili inaopata kutoka kwa wadau,” amesema Biteko.
Amewahakikishia wadau hao wa kimataifa kuwa hakuna fedha yoyote kwenye mradi huo itakayopotea, huku akiwataka viongozi wa Serikali za mitaa kutekeleza shughuli zote ambazo ni kipaumbele cha kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
”Niwahakikishie kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha mradi huu unafanikiwa. Nataka nitoe hakikisho kwamba uwekezaji huu hautapotea, na hakuna fedha yoyote hata senti ambayo imewekezwa hapa itakayopotea,” amesema Biteko.
Akizungumzia mradi huo, amesema umekuja kwa wakati sahihi kwani kutokana na jiografia ya Tanzania ambayo imezungukwa na nchi za maziwa makuu ina hatari ya kushambuliwa na magonjwa ya kitropiki ikiwemo homa ya bonde la ufa, kuvuja damu kwenye pua, na hivyo kuwa tishio kwa afya ya wananchi.
Amesema kwa mujibu wa ripoti ya WHO Kanda ya Afrika mwaka 2023, kati ya mwaka 2001 Hadi 2022 Afrika imekumbwa na milipuko ya magonjwa takribani 2,134 sawa na milipuko 102 kila mwaka, ambapo uwepo wa majanga hayo unahitaji mikakati ya pamoja, hivyo, uzinduzi wa mfuko huo unaunganisha nguvu za wadau na kuleta matokeo ya uhakika.
”Hivi karibuni tumeshuhudia milipuko ya magonjwa kama Uviko-19 uliokuwa na visa 38,709, Maaburg (visa tisa na vifo vitano), pia kipindupindu, sumukuvu, kimeta, na chikungunya ambayo yametuondolea nguvu kazi ya taifa, tunapaswa kuwa na mikakati imara ya kukabiliana nayo,” amesema Biteko.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema mradi huo utanisaidia kuimarisha uwezo wa kukinga, kugundua na kudhibiti magonjwa yote ya mlipuko ambayo yanatishia uhai wa nchi na mipaka ya Kikanda, ambapo Serikali itaimarisha mifumo yake ya afya kudhibiti maradhi hayo.
”Tunakwenda kuimarisha mifumo yetu kwa kujenga vituo vya dharura (Isolation center), kuimarisha udhibiti wa magonjwa haya kwenye maeneo yote ya mwingiliano, mifumo ya upatikanaji maji safi na salama, upatikanaji wa taarifa kwa haraka kuanzia ngazi ya jamii mpaka mikoa, maabara zetu ziwe na uwezo wa kufanya vipimo kwa haraka na kutoa matokeo sahihi,” amesema Dk Magembe.

Baadhi ya wadau wa afya jijini Mwanza wakishiriki katika hafla ya uzinduzi wa mfuko wa kukabili magonjwa ya mlipuko (Pandemic Fund in Tanzania), leo jijini Mwanza.
Dk Magembe amesema magonjwa yanayotishia uhai wa dunia kwa sasa ni yale ambayo yanatoka kwa wanyama, ndege, mimea na viumbe wengine na kwenda kwa binadamu hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inayo mifugo na wanyama wengi ambao wanaweza kuwa chanzo cha magonjwa hayo ya mlipuko.
”Tunaamini kwa muda wa miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huu tutapata matokeo makubwa na yataiweka nchi yetu kukaa mahali salama na kuwa na uwezo wa kujizatiti dhidi ya magonjwa ambayo yanaisumbua jamii. Na kila fedha iliyopangwa tutaisimamia ilete matokeo yaliyokusudiwa,” amesema Magembe.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali imeimarisha huduma ya afya mkoani humo kwa kuwekeza takribani Sh62 bilioni katika sekta ya afya.
”Katika kipindi hicho kuna ongezeko kwenye dawa na vifaa tiba, awali tulikuwa tunapokea Sh4 bilioni lakini katika kipindi hiki hadi mwaka huu sasa tunapata fedha takribani Sh10.3 bilioni kwa ajili ya dawa na vifaatiba,
tumeongeza vituo vya afya vyenye uwezo wa kufanya upasuaji vimefikia 45 kutoka vituo 17,” amesema Mtanda.