Siku tano baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuufungulia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, shirikisho hilo leo Jumatano, Oktoba 15, 2025 limetangaza kuvifungia viwanja vya Sokoine, Mbeya na kile cha Liti, Singida.

Taarifa iliyotolewa na TFF leo imefafanua kwamba viwanja hivyo vimefungiwa kwa vile havijakidhi vigezo vya kikanuni kutumika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia uwanja wa Liti, Singida kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

“Miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.

“Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika

kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF,” imefafanua taarifa ya TFF.

TFF pia imeufungia Uwanja wa Sokoine, Mbeya huku ikizitaka klabu kuboresha miundombinu ya viwanja.

 “Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia uwanja wa Sokoine, Mbeya kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

“Miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.

“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” inafafanua taarifa ya TFF.

Uwanja wa Sokoine unatumiwa na timu za Mbeya City na Tanzania Prisons na Uwanja wa Liti unatumiwa na timu ya Singida Black Stars.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *