
Agosti 28, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilipuliza rasmi kipyenga cha kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari muhimu ya kidemokrasia ambayo Watanzania wanapewa nafasi ya kuchagua viongozi watakaowaongoza katika ngazi zote za uongozi wa umma.
Na sasa tunaelekea dakika za lala salama, kwa sababu tumebakiza takribani wiki mbili tu, tuhitimishe kampeni na Jumatano ya Oktoba 29, 2025, Watanzania watapiga kura kuwachagua viongozi wao watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo.
Rai yangu kwao ni kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki, kilichosalia kwa kusikiliza kampeni za vyama vyote na hatimaye kufanya uamuzi mzuri siku ikifika ya kupiga kura. Katika kipindi chote cha kampeni, makala zangu zilijielekezwa kwenye kutoa elimu ya uraia kuhusu umuhimu wa uchaguzi. Nililenga kuchambua ilani za vyama vya siasa ili kumsaidia kila Mtanzania kwenda kwenye chama au mgombea fulani kwa sababu mahsusi, si kwa mkumbo, bali kwa kufanya uamuzi makini.
Somo la kwanza na la msingi zaidi katika safari ya uchaguzi ilikuwa kuelewa thamani ya kura yako. Katika taifa lolote, kitu chenye thamani kubwa ni mwananchi.
Mwananchi ndiye mmiliki wa nchi, katiba na mamlaka yote ya kitaifa. Kwa hivyo wewe, kama Mtanzania, ni mwenye dhamana kubwa; una mamlaka, heshima na thamani ya pekee.
Thamani ya kwanza kubwa kwa mwanadamu ni uhai na afya njema, ambayo ni zawadi ya Mungu. Thamani ya pili ni haki ya uraia, haki yako ya kuwa Mtanzania, ambayo haiwezi kuondolewa na yeyote.
Thamani ya tatu na yenye nafasi kubwa baada ya uraia, ni haki ya kupiga kura na haki ya kugombea kuchaguliwa. Hivyo basi, kura yako ni urithi wenye thamani kuu.
Ni bahati mbaya kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakieneza uwongo ili kuwakatisha tamaa wananchi wasishiriki uchaguzi.
Wapo wanaodai kwamba siku ya kupiga kura uchaguzi hautafanyika, eti kutakuwa na maandamano ya taifa nzima yanayolenga kuuzuia.
Haya ni madai ya uwongo wa mchana kweupe. Ukweli ni kwamba kura yako ndiyo silaha halali ya kidemokrasia inayokuwezesha kumuajiri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani.
Kwa kura yako, unamwajiri kiongozi. Kwa kodi zako, unamlipa mshahara wake. Hata kama rais anaonekana kuwa mtu wa juu, kwa hakika ni mtumishi wako. Wewe ndiye bosi halisi. Na japo mshahara wake na wa serikali yake hulipwa kwa kodi zako, kumbuka kuwa wewe ndiye chanzo cha mamlaka hayo.
Kwa msingi huo, kila aliyejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura anapaswa kutunza kadi yake ya kura. Kadi hiyo ndiyo silaha yako ya kidemokrasia.
Hapo nchi jirani ya Kenya, kadi ya kura huitwa kichinjio, ikimaanisha chombo cha kumchagua kiongozi mzuri na kumwondoa yule mbovu. Sisi pia tunapaswa kuitunza kadi hiyo hadi Jumatano Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi.
Ni muhimu kufahamu kuwa kujiandikisha kupiga kura ni hiyari na hata kupiga kura yenyewe ni hiyari ya mtu.
Hata hivyo, usiposhiriki, bado unaendelea kubeba jukumu la kulipa kodi zinazowalipa viongozi waliochaguliwa na wengine.
Kwa hiyo, usipopiga kura au ukapiga kura, bado utakatwa kodi. Swali ni; kwa nini ukubali kulipa kodi za kiongozi ambaye hukuchagua? Kuchagua ni fursa ya kuondoa maumivu hayo. Unapomchagua kiongozi unayemwamini, unapata furaha na hamasa ya kulipa kodi, kwa sababu unajua fedha zako zinamsaidia kiongozi uliyekubaliana naye kisera.
Ni kweli pia kuwa kuamua kugombea nafasi yoyote ya uongozi ni hiari ya mtu binafsi au chama chake. Hakuna anayelazimishwa.
Lakini ikumbukwe ni kosa kisheria mtu au chama kuzuia au kushawishi wananchi wasitumie haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi.
Katiba ya Tanzania kupitia Ibara ya 5 na 21 inatambua haki ya kupiga kura na kuchaguliwa kama haki ya msingi ya kila Mtanzania.
Kwa kuwa kushiriki uchaguzi ni hiyari ya kila chama au mtu, basi asiyetaka kushiriki asiwe chanzo cha kuzuia wengine. Ni wajibu wa vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu, kuwasilisha sera zao na kushindana kwa hoja, si kwa vitisho. Wananchi wanapaswa kupewa nafasi ya kusikiliza, kutafakari na kuamua kwa uhuru bila ushawishi haramu.
Kura yako ni chombo chenye thamani kubwa mno. Ndiyo sauti yako, nguvu yako, na mamlaka yako. Usikubali kusukumwa kando na propaganda wala vitisho.
Jitokeze kusikiliza kampeni, shirikiana na wengine kujadili sera na hatimaye, tumia kura yako kuchagua viongozi bora watakaokutumikia.
Demokrasia imara hutegemea wananchi wanaotambua thamani ya kura zao. Kila Mtanzania mwenye umri wa kupiga kura anapaswa kutambua kuwa kushiriki uchaguzi si wajibu wa kifedha pekee, bali pia ni wajibu wa kimaadili kwa taifa. Kwa hiyo, jihimu kutumia kura yako kama silaha ya kikatiba na ya kidemokrasia kwa manufaa ya taifa letu.
Kura yako, thamani yako.
Mungu Ibariki Tanzania.