
WAKATI Ulaya meneja katika timu ndiye bosi wa benchi la ufundi akiwa na majukumu ya kusimamia na kuongoza shughuli zote za kiufundi kuanzia usajili wa wachezaji, uandaaji na usimamiaji wa timu katika ligi, kuzungumzia masuala yote ya kiufundi ya timu na mengine yanayohusiana nayo, hapa kwetu imekuwa tofauti kwa mujibu wa kanuni za Shi-rikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kutokana na kanuni hizo za TFF, ni wazi Dimitar Pantev wa Simba anabanwa kufanya shughuli za kuiongoza timu hiyo huku jukumu likibaki kwa Seleman Matola ambaye anasimama kama kocha mkuu kwani ana vigezo vyote vina-vyohitajika.
Wakati Matola akisimama kwenye benchi la Simba kuanzia mechi za mashindano ya ndani na ya kimataifa akiwa ana-tambulika kama kocha mkuu, msaidizi wake ni Simeonov Boyko Kamenov ambaye alitua siku moja na Pantev.
Hata hivyo, Pantev anaweza kuukwepa mtego huo muda wowote akiingia tu darasani kwa nia ya kusaka leseni ya UEFA Pro ambayo kwa kawaida inachukua kipindi cha takribani miezi 12 hadi 18. Kwa mujibu wa sheria, kocha ambaye hana sifa zinazotakiwa, akianza tu masomo (sio hadi amalize), anaruhusiwa kuiongoza timu.
KANUNI ZINASEMAJE?
Kanuni ya 77 za Ligi Kuu Tanzania Bara toleo la 2025 kuanzia kipengele cha kwanza hadi cha nne, kinazungumzia vigezo vinavyotakiwa kwa makocha.
Kipengele cha kwanza kinasema: “Kila klabu inapaswa kuajiri Kocha Mkuu na wasaidizi wenye sifa na ujuzi kwa timu ya kwanza (wakubwa) na za vijana (U20 na U17) wanaokubalika kwa mujibu wa taratibu za TFF na mikataba yao kusajiliwa TFF.”
Kanuni hiyo inaendelea kipengele cha pili kwa kubainisha: “Kocha kutoka nje ya nchi atathibitishwa kwanza na TFF kwa kuzingatiwa pia kupatikana kwa kibali stahili cha kuishi na kufanya kazi nchini kabla ya kuingia mkataba na klabu.
“(3) Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na angalau Diploma A ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya mabara mengine yanayotambuliwa na FIFA. Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na angalau Diploma B ya CAF au inayolin-gana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya mabara mengine yanayotambuliwa na FIFA.
“3.1 Kocha mkuu wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau Pro Diploma au inayolin-gana nayo. 3.2 Kocha msaidizi wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau A Diploma au inayolingana nayo. 3.3 Kocha wa timu ya Ligi Kuu kutoka nje ya Tanzania ni lazima awe amefundisha klabu ya Ligi Kuu au timu ya Taifa katika nchi yoyote ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“(4) Kocha Mkuu ndiye mkuu wa shughuli zote za kiufundi za timu kuanzia usajili wa wachezaji, uandaaji na usimamiaji wa timu katika ligi, kuzungumzia masuala yote ya kiufundi ya timu na mengine yanayohusiana nayo.”
KWA PANTEV IPOJE?
Pantev mwenye umri wa miaka 49, ana leseni ya UEFA A ambayo kwa mujibu wa kanuni za TFF na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), hawezi kuiongoza timu kama kocha mkuu kwenye mashindano yao.
Kwa upande wa Matola ambaye wakati Simba inafundishwa na Fadlu Davids kabla ya kuondoka hivi karibuni alikuwa kocha msaidizi, lakini ana leseni ya CAF A, inayomuwezesha kuiongoza timu kama kocha mkuu.
Simba kwa sasa inajiandaa na mechi ya mkondo wa kwanza ya hatua ya pili ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, Oktoba 19 mwaka huu.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Somhlolo uliopo nchini Eswatini, kisha marudiano ni Oktoba 26, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla anafuzu makundi.
NSINGIZINI YATOA MSIMAMO
Nsingizini Hotspurs baada ya kuiondosha Simba Bhora katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa faida ya bao la ugenini, imesema inahitaji kuendelea kufanya vizuri kuweka rekodi mpya.
Timu hiyo katika mechi ya kwanza hatua ya awali ugenini dhidi ya Simba Bhora ya Zimbabwe, ilipata sare ya bao 1-1, kisha nyumbani ikawa 0-0. Ikafuzu.
Akizungumzia mechi ijayo dhidi ya Simba SC, Afisa Uhusiano wa Umma wa Nsingizini Hotspurs, Mnotfo Nkosi, ames-ema: “Timu iko tayari, na tunawaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono wachezaji. Hii ni hatua kubwa kwa soka la Eswatini.”