
Kampeni zinazidi kupamba moto wakati muda unakwenda kwa kasi kama treni ya umeme. Tumebakiza siku chache kuingia kwenye maboksi ya kura. Hata hivyo kadiri muda unavyoenda, tunaongeza vibonzo na kupunguza umakini wa sera.
Mwanzoni tulianza na vibonzo, kati tukabadilika na kusikia sera. Kwa mawazo yangu nilidhani wasindikizaji wameshachoka, lakini huku mwishoni vibonzo vimerudi tena. Labda wamepata ufadhili mpya.
Kitu kikubwa kisicho na maswali ni amani ya nchi ambayo vyama vinaihubiri. Lakini naona mapungufu makubwa kwenye ahadi zinazotolewa na wagombea wengi.
Wananchi hawaoni taabu kushangilia kila ahadi, na sababu zipo wazi kabisa: kwanza hawana kazi wala kipato, na mtu wa hivyo hufikiria kujisahaulisha matatizo yake kwa namna yoyote. Ukimwambia “kila mtanzania atamiliki ndege” atashangilia kupunguza msongo.
Ndio maana tukawaomba waandishi wa habari wanaosafiri na kampeni, waulizie maswali kwa niaba ya wananchi. Ahadi hizi tunazozisikia leo ni mwendelezo wa zile zilizokwisha kutolewa miaka chungu nzima iliyopita.
Tujue ni vitu gani vilivyokwamisha ahadi hizo kutekelezeka pale mwanzoni, na wagombea wapya watafanya mbinu zipi mpya katika kutimiza ahadi zao. Kila mmoja anakiri kuwa watanzania si masikini, lakini umasikini unalipo.
Kuna wakati nikiangalia kampeni za wagombea urais, ubunge na udiwani, huwa najisahau na kudhani naangalia shoo ya komedi. Ninaporudi kwenye hali ya kawaida na kuwatazama wagombea, nafikiria kwamba wengine ni wachekeshaji waliochelewa kupata fursa katika tasnia hiyo.
Nafikiria hivyo kwa sababu zamani hakukuwa na majukwaa ya vichekesho hapa nchini hasa ukizingatia kwa wakati huo sanaa haikupata kuwa ajira.
Kwa masikio yangu nilimnasa mgombea mmoja aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa akipata nafasi ya urais, atapiga marufuku matumizi ya vitanda vya futi sita kwa sita.
Alisema kuwa vitanda hivyo vimekuwa sawa na viwanja vikubwa vinavyosababisha wachezaji wasikutane. Aliongeza kuwa vitanda hivyo vinaongeza uvivu wa watu kuzaana, hivyo katika utawala wake ataruhusu vitanda vya upana wa futi nne au pungufu.
Nilijiambia kuwa kabla ya kucheka niingie ndani zaidi, kwani hata yule aliyekazia sera ya “ubwabwa” alikuwa na ufafanuzi wake. Ni kweli kuwa japokuwa idadi ya watu imeongezeka duniani, labda mwenzetu alitazama jinsi Watanzania wanavyopoteza nguvu za kuzaana. Labda ningemwelewa iwapo angeeleza namna ya kupambana vyanzo vya udhaifu wa uzazi kama msongo, vyakula vya hovyo na kadhalika.
Mwingine aliyenifurahisha alikuwa akizindua kampeni kwenye uwanja wa nyumba. Nimegundua kuwa unaweza kuwaalika watu pilau la mchana kwa masharti ya kula baada ya kukupigia makofi.
Mchawi ni TV tu; ikishasoma kuwa umezindua basi imetoka hiyo. Ulipofika wakati wa kupiga picha ya pamoja mbele za waandishi, sikumwona mwandishi bali viongozi walichomoa simu zao na kupigana picha.
Yupo mgombea alitaka kusoma ilani ya chama chake, lakini akasahau alipoiweka.
Kama sikosei ilani hiyo aliiandika akiwa ndani ya gari akaisahau humo. Tena bahati yao wamepewa magari, vinginevyo angeiandika kwenye mgongo wa bodaboda! Basi mgombea akapepesa macho pale uwanjani bila kuiona.
Akamwuliza mgombea mwenza, lakini bado haikusaidia: akaipotezea ilani na kuunga stori ingine papo hapo.
Mwingine alikuwa akizindua kampeni zake kule Mtoni Kijichi. Alisema kuwa iwapo atapewa ridhaa ya kuwa Rais, atajenga meli yenye urefu wa kuanzia Mtoni Kijichi hadi Posta.
Nilipata picha kuwa mgombea huyo angezindulia kampeni zake Chanika, basi angetuambia urefu wa meli ungeanzia Chanika hadi Posta. Baadaye aliilaani mikopo ya ‘kausha damu’. Huyu alidai laiti angeukwaa urais angeikomoa mikopo hiyo kwa kuibadili kuwa mikopo ya ‘ongeza damu’.
Mwingine tena ameahidi mara tu atakapoingia Ikulu kule Zanzibar atajenga vinu viwili vya nyuklia. Inaonekana kuwa wapinzani wengi (au tuseme wengi kati ya waliosalia) wanajua mahitaji ya watu kwa sasa. Watu wana njaa unawaahidi nyuklia…
Ndiyo maana idadi ya wapiga kampeni inazidi ya wananchi wanaokuja kusikiliza sera. Viongozi na wanachama wao ndio wanaoshangilia na kujitokeza kuchukua kadi kwa mara nyingine.
Kuna kila dalili za kambi ya upinzani kufeli kirahisi. Hali hii inaonesha kuwa njia ni nyepesi sana kwa chama tawala kilichojizatiti kiuchumi.
Lakini pia ni jawabu kuwa habari zinazosikika kuwa wananchi wameimarika kiuchumi si za kweli. Viongozi mngeliona hili kwenye engo ya mtu wa kawaida, mngeng’amua kwamba mlikuwa mkidanganywa na wawakilishi wenu waliokuwa wakinuia kubaki kwenye nafasi zao.
Kuna hatari ya wananchi kuiona siasa kama adui yao mkubwa katika maendeleo yao. Hii ni kwa sababu ahadi mpya wanazopewa na wanasiasa hazikidhi kutokomeza shida zao.
Watu hawana uwezo, hata wale walioajiriwa wanashindwa kupata milo kamili, matibabu bora, wanashindwa kusomesha watoto na kubaki wakitinga kwenye vitanzi vya madeni. Badala ya wagombea kuwaonesha njia watakazotumia kuwakwamua, wanawaongezea msongo.
Masikini wengi wameumizwa na mikopo. Unapomwambia ati njia ya kumkwamua ni kumwongezea mikopo, unamweka kwenye hali ngumu akikumbuka mateso yaliyomganda.
Ni bora neno hilo lisitajwe kabisa na wagombea kwenye kampeni zao. Watu waoneshwe kwamba wanaweza kujitegemea, mikopo iwe kwenye mambo ya ziada tu. Mtu aweze kujenga nyumba yake, mikopo iwe kwa ajili ya kuipendezesha tu.