Nilirejea kwa mbambamba na mbwebwe na Bi Nkubwa na vitoi tulivyovitengezea huku lau ndugu wavijue na vijuane visije, siku moja, kupelekeana mashambulizi na posa mabuda tukaonekana hamnazo au kujitoa ufahamu kama yule kiherehere wa Msonga.

Hayo tuyaache. Baada ya kupoa kwa mwezi mmoja na ushei, niliamua kutia timu tena ughaibuni kuendelea na kubeba maboksi kama kawa. Unatokaje Bongolalaland bila lau kubebea vitu vya kibongo?

Watoi watakwendaje kuwaringishia wenzao bila vitu vya bongo ili kuonyesha kweli stori zao si rongorongo za kitoi au kutafuta ujiko usipopanda kama mwanasiasa na wachunaji wauzao neno kwa roho na uroho mtakakitu? Bila kutonywa, si tukaingia zetu kule wanapokalia koo aka vururu vururu vurugu mechi ya bodaboda na ndinga na maduka yaliyojaa hadi mashimoni na joto.

Si unajua tena. Mafyatu wa kibongo ukigoma kuchunwa, wanauchuna ili washenzi wa Kalia koo na kwengineko wakunyonyoe wahondomole. Bila kuchelea mtima nyongo huu, we! Si tukaingia kwenye duka la gabachoooli mmoja aliyetupokea kwa bashasha kana kwamba huwa hatubagazani, hatubanangana, na kubaguana!

Kwa vile haya tushayazoea ughaibuni ambako watasha wabaguzi hutuita watu wa rangi aka people of colour kama signal ya kutubagua, tulimpuuzia na kuendelea kile kilichotupeleka, yaani kunua chocolate na kumuachia usanii wake ulioficha ubaguzi na unyama na kuishia kivyetu.

Hata hivyo, tulijifunza kitu. Wabongo wengi hawajui biashara. Ukienda dukani kwake, badala ya kukuchangamkia, anakuona kama umeenda kubomu au huna duka kama yeye wakati wote mna shida, yeye njuluku yako, nawe bidhaa au huduma yake. Kiduka chake kipo mtaa wa kwanza au wa pili kutoka Shimoni Sokoni kuelekea Mnazi Mmoja. Ni mtaa uliojaa maduka yaliyosongamana. Kwa vile tulikuwa tumehamanika na kufurahia kupata hii kitu, si tukasahau kuangalia tarehe ya kuisha matumizi!

We! Nani anaweza kuamini kuwa tuliuziwa chocolate zilizoexpire mwaka 2022? Ni roho mbaya na ulafi kiasi gani?!

Baada ya kufyatuliwa hapo kwenye chocolate, tulikwenda kununua dhahabu za Bi Mkubwa ili naye akawaringishie wenzake kazini. Tulipiga guu hadi maeneo ya mtaa wenye Jina la waziri mkubwa wa India aliyeuawa kwa kutwangwa shaba.  Kuna huyu Msomali. Anatuchangamkia kwa basha na kutupunguzia bei. Tulifurahi sana. Tulinunua dhahabu ya madafu milioni kumi na ushei. Guess what? Kumbe alipotukaribisha kwa bashasha hakumaanisha kutupenda au kutushobokea zaidi ya kujenga mazingira ya kumsaidia kuminya kodi!

Baada ya kupata bangili, hereni, mikufu na vikuku, si jamaa akatuambia bei. Tulilipa bila kuuliza hasa ikizingatiwa kuwa madafu siku zote yako chini mbele ya dolari.

Baada ya kumkatia chake, tulitaka atupe risiti. We! Jamaa alitushangaa na kuuliza “nyie wageni hapa?” Nami nilimuuliza alikuwa akimaanisha nini? Alijibu bila aibu “kwanini mnataka risiti wakati tunaweza kuwaandikia certificate na kuwapunguzia mambo yakaisha?” Kwa ushamba wake wa ughaibuni, Bi Mkubwa alidakia “why should we do that!” Kusikia hivyo, jamaa alizidi kucheka kwa tunavyogtindiganya mambo! Mie nilishangaa nisielewe kwanini alikuwa akinicheka kwa swali la kizalendo kama hili? Nilidakia? Wewe iko Tanzania au somali?

Kama iko Tanzania, sasa zalendo iko wapi? Yule muuza dhahabu alizidi kucheka na kusema “kaka wazalendo wako wapi nchi hii? Kweli wewe ni mgeni.”

Nijifyatua na kujifanya sijamuelewa. Jamaa alisema “umeona misongamano na uvunjaji wa sheria wakati unakuja hapa? Kabla sijajibu, aliniuliza “unaishi wapi hapa mjini?” Nilimjibu “Mikocheni.”

Alisema “alaa! Kumbe hujui ugumu wa maisha hapa mjini siyo?” Kukatisha hadithi ndefu, jamaa anifyatua shule ya bure nikajiona kama bongolala.

Alisema kuwa ni kweli wanakwepa kodi. Je wanaotaka walipwe kodi zaidi ya kuzifyatua, wanazifanya nini huku kuacha mafyatu washi kana kwamba hawana lisrikal? Kuona hivyo, nilikubaliana naye, mambo yakaishia hapo japo, hadi leo, roho inaniuma nikishindwa kumlaumu au kujilaumu kwa sababu, kama kungekuwa na waongozaji wazalendo, nisingekubali kushiriki uhujumu huu.

Baada ya kununua bling bling za Bi Mkubwa, tulikwenda zetu mitaa ya Msimbazi kununua zawadi za wakwe zangu na jamaa wengine. Kila tuliponunua vitu kama vile microwave, blenders, na madudu mengine ambayo ni top secret, hakuna aliyetupa risiti zaidi ya kutupunguzia bei na kumalizana hapo hapo. Je, kwa mchezo huu, kaya inapoteza kodi kiasi gani? Hata ingeipata, ingepigwa kiasi gani na wajanja walioko kwenye ulaji? Hivi tunamkomoa nani

Maswali ya waria yalinifikirisha. Je, kodi wakilipa wanapata mrejesho sawa wa faida na matumizi yake? Ughaibuni, hulazimishwi kulipa kodi. Utalazimishwaje wakati faida na matumizi yake unayoana na kuyahisi kila mahali? Inashangaza kuona mafyatu wanene wachache wanaishi peponi wakati wengi wakiishi motoni tena pa kutengenzwa na hao hao waishio kwenye pepo waliojitentgezea! Hivyo ndivyo wabongo walivyonifyatua. Roho inauma we acha tu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *