Katika eneo la Dagoreti lililoko kaunti ya Nairobi, nchini Kenya Cecilia Wanjala, mkulima kutoka eneo hilo anaeleza mchango wake kwa jamii na anaanza kwa kueleza ni vile ambavyo anaweza kukimu mahitaji ya familia yake.

“Wanawake wanaleta mabadiliko vijijini kwa kuendeleza biashara, kilimo, na ufugaji. Kupitia biashara na ukulima nimeweza kulipa ada ya shule, ninawezakununulia watoto chakula, na kumudu mahitaji ya hospitali. Ninasimamia familia yangu kwa kuuza mboga, na pesa ninazopata natumia kukimu mahitaji yao.”

Licha ya kujitahidi kukwamua familia yake, Cecilia ana ombi kwa serikali ili aweze kujiendeleza zaidi.

“Naomba serikali itusimamie tukiomba mkopo ili tuendeleze biashara. Ni vigumu sana kwa wanawake kupatiwa mkopo, sio rahisi.”

Nakutana na mwanamke mwingine wa kijiji eneo la Kikuyu hapa hapa Dagoreti, naye si mwingine bali ni Mercy Meliki, mkulima na mfanyabiashara. Anaeleza ni kwa vipi ameweza kusimama na familia yake. 

“Nimeweza Kumudu mahitaji kwa familia yangu kupitia biashara, Ninauza mahindi na kuweka pesa kidogo, zingine natumia kulipa karo ya shule, na pia kunuwa chakula kwa nyumba. Pia naweka pesa kidogo kwa chama cha wanawake.”

Katika siku hii maalum, Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya  Wanawake UN Women kupitia wavuti wake limesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua thabiti na za haraka ili kuhakikisha kuwa wanawake wa vijijini wanapewa nafasi sawa, haki zao zinalindwa, na wanapewa uwezo wa kuongoza mabadiliko  katika jamii zao ili kufanikisha Malengo ya Maendelevu SDGs.

Nikamuuliza Mercy iwapo ana ombi lolote kwa serikali au Umoja wa Mataifa siku hii ya mwanamke wa kijijini

“Ombi langu kwa serikali na kwa Umoja wa Mataifa ni kwamba, serikali waweze kutupatia mikopo, tuweze kuendeleza na kupanua biashara na kilimo. Kwangu mimi sijawahi kukatazwa mkopo, sijakuwa na changamoto yoyote nilipewa mikopo kwa urahisi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *