Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limeeleza kuwa Oktoba 29, 2025, wananchi wote wana haki ya kikatiba ya kwenda kupiga kura bila hofu, huku likionya vitendo vyovyote vya kutisha au kujaribu kuwasababisha hofu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 15, 2025 Kamanda Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa vitendo vya kutishia wananchi havikubaliki na vinaingilia haki ya kikatiba ya kila mwananchi.

“Tarehe hii haikuja yenyewe, ipo kisheria ipo kikatiba na watu wana haki ya kwenda bila hofu kupiga kura na kuchagua mtu yeyote wanayemtaka,”amesema Muliro.

Amesema vitendo vya kujaribu kutishia watu havikubaliki kwa sababu shughuli hiyo ni ya kisheria. Jeshi la Polisi litaendelea kufuatilia, kuzuia, kubaini na kutanzua matishio yote ya kiusalama na siku hiyo watu watatimiza jukumu lao la kikatiba bila hofu.

Mbali na hilo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kisheria limefanikiwa kuwakamata watu wanne kwa tuhuma za kuendesha televisheni mtandao bila kuwa na leseni.

Muliro amesema kati ya Oktoba 3 na 4,2025  jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wakiendesha televisheni mtandao bila kuwa na leseni.

“Kama mnashuhudia sheria imeruhusu kuwepo kwa vyombo vya habari lakini kwa kufuata misingi ya kisheria ya jinsi ya kuendesha vyombo hivyo,”amesema Muliro.

Amesema waliokamatwa ni Japhet  Thobias na Joseph Mabwe, wote wakazi mkazi wa Sabasaba, Ukonga, wanaodaiwa kumiliki WISPOTI TV,

Wengine ni Tegemeo Mwenegoha, mkazi wa Tabata, Ilala, mmiliki wa TV Media Two pamoja na Elia Pius, mkazi wa Mbezi Juu, Kinondoni, mmiliki wa Costa TV.

Amesema watu hao wanamiliki media hizo kinyume cha sheria bila kusajili na kuendesha shughuli zao kinyume na sheria pia. Nchi hii inafanya shughuli zake kwa kufuata misingi ya kisheria.

Amesema shughuli zozote ambazo zinafanyika kinyume cha sheria ni makosa na kwa sababu hiyo wamehojiwa wamekamatwa na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

“Upelelezi umekamilika na  mifumo mingine ya kisheria itatumika kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mahakamani haraka kadri itakavyowezekana,” amesema Muliro.

Muliro amesema wamefuatilia mara ya kwanza jambo la kwanza zinapopatikana tuhuma ni kupeleleza kwa hiyo uchunguzi umefanyika.

Aidha, Polisi imewatahadharisha wananchi kuendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na mifumo ya kisheria, huku ikisisitiza kuwa haitasita kuwachukulia hatua wote wanaotuhumiwa kutenda makosa.

“Jeshi la Polisi halitasita kumtia mbaroni mtuhumiwa yoyote ambaye atabainika anafanya vitendo vya kihalifu ambavyo ni kinyume cha sheria. Tunapenda kuwahakikishia wananchi jeshi linafuatilia matendo na matamko mbalimbali. Pia tunawahakikishia jiji lipo salama na litaendelea kuwa salama,”amesema Muliro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *