
Jarida la L’Express de Madagascar, limeripoti kwamba, kocha Romuald Rakotondrabe maarufu kwa jina la Rôrô, jana Oktoba 14, 2025, ametua jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya kujiunga na klabu ya Yanga.
Taarifa zinabainisha kwamba, kocha huyo aliyetokea Madagascar kuja Tanzania, alitua jijini Dar es Salaam jana usiku akiwa amepewa mkataba wa miaka miwili kuifundisha Yanga ukiwa na kipengele cha kuongeza.
“Ni klabu bora zaidi Tanzania na moja ya zenye mafanikio makubwa Afrika,” amesema Roro alipozungumza na jarida hilo.
Alipoulizwa kama amefurahishwa na masharti ya mkataba aliopewa, Roro amejibu: “Mambo muhimu katika mkataba ni pamoja na mshahara ambao kwanza kabisa unaniridhisha. Kisha, viongozi wa klabu wameahidi kuhakikisha mahitaji yote ya timu yanatimizwa kwa hali bora. Nitapewa sehemu ya kukaa na gari kwa ajili ya matumizi yangu ya kila siku.
“Aidha, nitaweza kusafiri mara mbili kwenda Madagascar katika msimu mmoja kwa gharama za klabu. Kuna maelezo mengine madogo nitakayoyajua nitakapofika. Hii ni klabu ya kitaalamu, kila kitu kimepangwa vizuri na kwa umakini.”
Katika hatua nyingine, Roro amezungumzia malengo ya klabu anayokwenda kuifundisha akisema: “Kama sikosei, klabu hii ilikuwa mshindi wa pili wa CAF mwaka 2022. Kwa muda mfupi, lengo kama walivyoniambia viongozi, na nitathibitisha nikifika ni kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika. Hilo ndiyo shabaha kuu ya klabu. Niliwauliza kama wana rasilimali za kutosha kufanikisha hilo, na wakanihakikishia kwamba wanazo kwa maana ya wachezaji, benchi la ufundi na uwezo wa kifedha.”
Roro aliyeiongoza Madagascar kumaliza nafasi ya pili katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Agosti 2 hadi 30, 2025, pia amezungumzia ishu ya kuachana na majukumu ya timu ya taifa.
“Nilikutana na Rais wa Shirikisho la Soka na maafisa wakuu wa serikali. Wote waliniunga mkono na kunitia moyo. Walisema ni fursa nzuri sana kwangu. Hakuna aliyepinga, hivyo nimeondoka bila wasiwasi wowote.”
Kuhusu madai yake ya mishahara ndani ya kikosi cha Madagascar, Roro amesema: “Viongozi tayari wamefanya jitihada zao. Mishahara yangu hadi Novemba 2024 imeshalipwa. Inabaki kuanzia Desemba 2024, ambayo bado nasubiri kutokana na hali ya kifedha ya sasa nchini.”
Alipoulizwa kama atakuwa tayari kurejea kuifundisha tena timu ya taifa endapo ataombwa kufanya hivyo, amesema: “Hilo litategemea pande tatu; klabu ya Tanzania, shirikisho, na mimi mwenyewe. Ikiwa maandalizi ya Barea (jina la utani la Madagascar) hayatapingana na ratiba ya ligi ya Tanzania au mechi za kimataifa, halitakuwa tatizo.
“Natoa mfano wa Nicolas Dupuis, aliyekuwa akiifundisha Barea huku akiwa kocha wa Fleury FC nchini Ufaransa. Kwa hiyo yote yatategemea mpango wa klabu. Ndiyo maana mkataba wangu umeandaliwa hivyo. Nafikiri itawezekana kufanya mazungumzo kuhusu hilo, mradi halitavuruga kalenda ya klabu. Kwa sasa, bado hatujafikia hatua hiyo, tutasubiri tuone baadaye.”
Kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro inayomuwezesha kufundisha timu yoyote inayoshiriki mashindano ya CAF na Ligi Kuu Bara, amekuwa na mbinu bora za kushambulia na kuzuia.
Katika mashindano ya CHAN 2022 nchini Algeria wakati Madagascar ikimaliza nafasi ya tatu, timu hiyo iliruhusu mabao matatu pekee katika mechi tano, ikifunga mabao tisa. Clean sheet mbili.
Katika CHAN 2024, Madagascar ilicheza mechi saba, ilifunga mabao tisa na kuruhusu saba ikiwa na cleansheet mbili pekee, huku timu hiyo ikimaliza nafasi ya pili ikipoteza mechi ya fainali dhidi ya Morocco kwa mabao 3-2.
Hivi karibuni, Mwanaspoti ilikujuza mpango wa Yanga kuwa kwenye mchakato wa kuachana na Romain Folz raia wa Ufaransa na kumpa dili Roro ambaye awali alifuatwa na timu za Al Merreikh na Simba, lakini akazikataa na kukubali dili la Yanga.
Mpango huo ulikuja kufuatia presha ya mashabiki waliyoielekeza kwa uongozi wa klabu hiyo baada ya kuona Yanga haichezi soka la kuvutia licha ya kutopoteza mechi yoyote ya mashindano msimu huu kati ya tano ilizocheza chini ya Folz, ikishinda nne na sare moja sambamba na kubeba Ngao ya Jamii mbele ya Simba.
Folz aliyetua Yanga Julai 14, 2025, katika mechi hizo tano zikiwemo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika akiivusha timu hiyo kutoka hatua ya awali na sasa inakwenda kukabiliana na Silver Strikers kuwania kufuzu makundi, jumla imefunga mabao tisa, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa ikimaanisha ina clean sheet tano.