ALIYEKUWA Skauti Mkuu wa Simba, Mels Daalder, ameteuliwa katika Shirika la R6 International Sports Agency na kwa sasa atajikita katika utambuzi na usajili wa vipaji vya kimataifa kwa niaba ya shirika hilo lenye makao yake Marekani.

Daalder aliyejiunga na Simba rasmi Mei 25, 2023, alijiuzulu nafasi yake ndani ya kikosi hicho, Oktoba 4, 2025, ikiwa ni wiki chache tu kupita tangu aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids kuondoka na kurejea Raja Casablanca ya Morocco.

Majukumu ambayo atakuwa nayo katika shirika hilo kubwa, ni uchunguzi na utambuzi wa vipaji na atatembelea mashindano mbalimbali, mazoezi na michezo ya ndani na ile ya kimataifa ili kutafuta wachezaji wenye vipaji vikubwa na vya kipekee.

Pia, atafuatilia wachezaji wachanga katika akademi, shule au timu ndogo ndogo, huku majukumu mengine ni kutumia pia mitandao ya kijamii, video na data kuchunguza uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, kama alivyokuwa anafanya akiwa na Simba.

Mbali na hilo, atafanya tathmini ya kiufundi kwa kuchambua uwezo wa mchezaji kama kasi yake awapo uwanjani, mbinu, stamina, uamuzi na uongozi, kisha kuandika ripoti ya tathmini kwa anayeonekana ana uwezo wa kujiunga na shirika hilo.

Jukumu lingine ni kutoa mapendekezo kwa wakurugenzi wa kiufundi au mawakala wa shirika hilo kuhusu wachezaji wanaofaa kuendelezwa au kuuzwa, jambo ambalo kwa Simba ilikuwa ngumu kupata nafasi hiyo hadi kuamua kujiuzulu mwenyewe kikosini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *