Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kupanua uhusiano na Uganda katika nyanja za kiuchumi, kilimo na biashara.

Seyyed Abbas Araqchi, ambaye yuko Kampala (Uganda) kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) amekutana na kufanya mazunguumzo na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.

Katika mazungumzo yake na Rais Museveni, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran sanjari na kuishukuru kwa Uganda kuwa mwenyeji bora wa mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa mshikamano na ushirikiano kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ili kulinda kanuni za msingi za harakati hiyo, kuzuia kudhoofika kwa utawala wa sheria, na kuunga mkono haki ya mataifa ya kujitawala.

Akiashiria umuhimu mkubwa ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia maanani katika kuimarisha uhusiano na Afrika, Araghchi amesisitiza utayarifu wa Iran wa kupanua uhusiano na Uganda katika nyanja za kiuchumi, kilimo na biashara.

Sayyid Abbas Araqchi pia amepongeza misimamo ya kimsingi ya Uganda ya kulaani hujuma za kijeshi za utawala wa Israel dhidi ya Iran.

Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni pia ameeleza kuridhishwa kwake na uhusiano wa muda mrefu kati ya Uganda na Iran unaozingatia kuheshimiana na manufaa, na kusisitiza azma ya nchi yake ya kuimarisha uhusiano na Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *