Lindi. Utafiti unaoendelea kufanyika katika Kitalu cha Lindi–Mtwara, mkoani Mtwara umeonesha dalili za uwepo wa gesi asilia, hususani katika vijiji vya Mnyundo na Mpapura, huku visima vya maji vikibainika kuvujisha gesi hiyo.

Utafiti huo unaojumuisha vijiji 48 katika eneo la takriban kilomita za mraba 736, vijiji 40 viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (Mtwara DC) na vijiji vinane viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama (Mtama DC).

Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya gesi na mafuta mkoani Mtwara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amesema utafiti wa awali unaonesha uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa gesi asilia katika eneo hilo.

“Kwa kutumia data za mitetemo zilizokusanywa awali, tumebaini kwamba kuna hadi asilimia 32 ya uwezekano wa gesi kuwepo katika kitalu hiki,” amesema Dk Mataragio.

Amesema mahitaji ya gesi yamekuwa yakiongezeka katika sekta mbalimbali zikiwamo za viwanda, majumbani na usafirishaji, jambo linaloifanya Serikali kuendelea kuchochea utafutaji na uendelezaji wa vyanzo vya nishati hiyo ili kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Katika ziara hiyo, Dk Mataragio pia ametembelea mradi wa kuongeza uzalishaji wa gesi katika eneo la Mnazi Bay, ambako amebaini kuwa mradi huo uko katika hatua ya maandalizi kwa asilimia 68.

Mradi wa Mnazi Bay unahusisha visima vitatu vya gesi asilia, Serikali inatarajia kuongeza uzalishaji kwa wastani wa futi za ujazo milioni 45 kwa siku kutoka kwenye visima viwili, huku kisima kimoja kikiwa ni kwa ajili ya utafiti zaidi wa uwepo wa gesi katika eneo lingine la kitalu.

Hivyo, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilishwa kwa mujibu wa ratiba ilivyopangwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema gesi asilia imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji mkoani humo na kwamba, uwepo wa miradi hiyo umechochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

“Kwetu sisi watu wa Mtwara, sekta ya nishati ni msingi wa maendeleo na usalama wetu. Nawapongeza TPDC na wadau wote kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya gesi asilia ambayo pia imetoa ajira kwa wakazi wetu,” amesema Kanali Sawala.

Mjiolojia, Paschal Njiko ambaye ni Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi kutoka TPDC, amesema shirika hilo litaendelea kusimamia makandarasi kwa karibu ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na ndani ya bajeti.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanamawa, Selemani Hassani ameishukuru Serikali kupitia TPDC kwa kuleta mradi huo kijijini kwao, na kueleza kuwa tayari wananchi wameanza kunufaika kupitia fursa za ajira na maboresho ya miundombinu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *