Nyota wa Barcelona, Eric Garcia, amemwagia sifu kocha wa Girona, Miguel Sánchez, kwa kumsaidia kurejesha kujiamini kwake, baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mkopo tangu msimu wa 2023–2024. 

Eric amefichua jinsi kocha huyo alivyomshawishi kucheza kama beki wa pembeni kwa ujanja katika mechi dhidi ya Cadiz, jambo lililomwezesha kukua zaidi kama mchezaji.

Akizungumza na SPORT, Eric ameeleza jinsi kocha Miguel alivyomshawishi acheze kama beki wa pembeni kwa mechi moja tu, lakini hatimaye akaishia kucheza nafasi hiyo msimu mzima wa La Liga. 

“Kweli, ilikuwa ni sehemu ya kujiamini niliyohitaji na ambayo kila mchezaji huitaji. Alinipa pia fursa ya kucheza zaidi upande wa pembeni, kucheza katika nafasi tofauti. Kabla ya hapo, nilikuwa ninasita kutoka kwenye eneo langu na akanidanganya kidogo. Siku moja dhidi ya Cadiz, aliniambia, ‘Leo tu utacheza hapa,’ na nilijikuta nikicheza hapo msimu mzima. Niliamini, na ilifanikiwa vizuri sana.” amesema Garcia.

GAR 01

“Sehemu kubwa ya mafanikio hayo ni kwa sababu yake, na nilimwambia hivyo wakati huo. Aliniamini wakati wengi hawakuwa na imani nami, na alinipa nafasi hiyo. Yeye ni kocha makini sana, anakuonyesha video nyingi ili kukuonyesha wapi unaweza kuboresha, na hilo lilikuwa muhimu sana kwangu.”

Eric Garcia anaweza kuikabili Girona ya Miguel wiki hii, ikiwa kocha wa Barcelona, Hansi Flick, atampa dakika za kucheza. Msimu wa 2023-2024, Garcia alicheza mechi 31 akiwa kwa mkopo Girona. Hata hivyo Eric Garcia alikataa kurejea Girona msimu uliopita.

Katika mahojiano hayo na SPORT, Eric Garcia amethibitisha kuwa alipewa nafasi ya kurejea Girona msimu uliopita, lakini akaamua kubaki Barcelona na kupigania nafasi yake chini ya kocha Hansi Flick.

GAR 02

“Mwaka jana, kulikuwa na kipindi nilikuwa sipati muda mwingi wa kucheza. Bila shaka, nilikuwa na chaguo la kurudi Girona, nilijua Michel yupo pale. Lakini mwishowe, nafikiri nilifanya uamuzi sahihi.”

Nyota huyo wa zamani wa Manchester City anaamini kuwa kiwango chake katika mechi dhidi ya Benfica kilikuwa ni hatua muhimu kwake chini ya Flick, kwani baada ya ushindi huo katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha alianza kumuamini zaidi.

Kwa sasa, Garcia yupo kwenye mazungumzo ya kuongezewa mkataba na klabu ya Barcelona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *