
Katika benchi la ufundi la Yanga linaloongozwa na kocha mkuu Romain Folz, vichwa vinauma wakati maandalizi kuelekea mechi ya ugenini ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silvers Strikers yakiendelea.
Kikosi cha Yanga ambacho kimeondoka leo Alfajiri Oktoba 16, 2025 kwenda Malawi kwa ajili ya mechi hiyo ya mkondo wa kwanza hatua ya pili dhidi ya Silver Strikers itakayofanyika Jumamosi Oktoba 18, 2025, unaambiwa Folz ameshapewa ramani ya eneo hatari zaidi kwa wapinzani hao.
Baada ya kupewa ramani hiyo, amekutana na wenzake wa benchi la ufundi na kutengeneza mkakati mzuri wa kushinda ugenini kwani anafahamu wakikosea kidogo tu, mambo yatakuwa magumu.
Akizungumza na Mwananchi, Folz amesema, imemchukua muda kidogo kuwafahamu wapinzani hao, lakini msaidizi wake, Patrick Mabedi aliyetambulishwa hivi karibuni amefanya kazi kuwa nyepesi.
Amesema Silver Strikers iko hatari sana eneo moja tu ambalo kwa Yanga pia ina watu wanaoweza kufanya mambo makubwa kutokana na viwango vyao.
“Nimepewa taarifa za Silver Strikers ni timu inayoundwa na wachezaji vijana na wanacheza kwa nidhamu sana, lakini ubora wao mkubwa upo kwenye eneo la kiungo.
“Kuwadhibiti lazima tutengeneze mpango wa kuvunja ubora wa safu yao ya kiungo, Yanga ina safu nzuri ya ushambuliaji ambayo imejipanga kuhakikisha inaulazimisha ukuta wa ulinzi kufanya makosa,” amesema.
Katika eneo la kiungo la Silver Strikers, Folz alisema amepewa jina la Uchizi Vunga ambaye mara kadhaa amekuwa akijumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Malawi kuwa ndiye mtu hatari zaidi.
“Nimepewa jina la kiungo wao bora anaitwa Uchizi Vunga, ni lazima tumdhibiti lakini pia nimemsoma naona kabisa kiwango chake hakijazidi tulionao hapa Yanga,” amesema Folz.
Uchizi ameichezea Silver kwa misimu mitatu huu ukiwa wa nne, akiwa na uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati na kiungo mshambuliaji, huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao saba kwa kipindi chote.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, ndiye amekuwa silaha mahiri ya kocha mkuu wa Silver Strikers, Peter Mgangira kwani amemtumia kwenye mechi zote za mashindano msimu huu sambamba na Levison Maganizo.
Katika kikosi cha Silver Strikers, mbali na nyota hao wawili, kocha Mgangira amekuwa akiwatumia zaidi kipa George Chikooka, Maxwell Paipi, Dan Sandukira, McDonald Lameck, Nickson Mwase, Stanie Davie na Chinsisi Maonga, ambao ndio waliocheza mechi zote mbili dhidi ya Elgeco PLUS na kuitoa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.