Wakosoaji wanasema Donald Trump anatumia ushuru kama silaha

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Daniel K
    • Nafasi, Mwandishi BBC

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, amekubali kusitisha ununuzi wa mafuta kutoka Urusi.

Trump amekuwa akisisitiza kwamba mataifa yanayonunua mafuta kutoka Urusi yanasaidia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kufadhili vita vya Ukraine. Amedai kuwa kuizuia Urusi kifedha ni hatua muhimu ya kukomesha vita hivyo.

“Vita vya Ukraine vilipaswa kuisha ndani ya wiki moja. Sasa ni miaka minne. Nataka vita hivi vikome. Sikuridhika India ikiendelea kununua mafuta kutoka Urusi. Leo wamenihakikishia kuwa hawatanunua tena. Hii ni hatua kubwa,” Trump alisema.

Alitoa kauli hiyo Jumatano alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani.

Pia unaweza kusoma:
Mvutano wa kibiashara unaendelea kati ya India na Marekani kuhusu ununuzi wa mafuta kutoka Urusi

Chanzo cha picha, JIM WATSON/AFP via Getty Images

Shinikizo la Marekani

Trump amekuwa akitumia suala la mafuta kama njia ya kuishinikiza India katika mazungumzo ya kibiashara.

India, hata hivyo, imepinga masharti hayo, hali iliyoleta mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Urusi huuza nje kiasi kikubwa cha mafuta na gesi. Wanunuzi wakubwa ni India, China na Uturuki.

“Tunapaswa kuishawishi China kufuata mkondo huo huo,” Trump aliongeza.

Serikali ya Trump pia imekuwa ikiishinikiza China na washirika wengine wa kibiashara kusitisha ununuzi wa mafuta kutoka Urusi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza mapato ya Urusi.

Trump alikiri kuwa India haiwezi kusitisha ununuzi huo mara moja, lakini alisema mchakato wa kusitisha unaendelea na utatekelezwa kwa hatua.

Ushuru mkubwa

Trump aliweka ushuru wa hadi asilimia 50 kwa bidhaa kutoka India. Aliueleza ushuru huo kama adhabu kwa India kwa kuendelea kununua mafuta na silaha kutoka Urusi.

Ushuru huo, ulioanza kutekelezwa mwezi Agosti, umetajwa na wanauchumi kama changamoto kubwa kwa uchumi wa India. Pia, ada ya ziada ya asilimia 25 imewekwa kwa miamala inayohusisha Urusi.

Trump alisema kuwa mapato kutoka mauzo ya mafuta ndiyo chanzo kikuu cha fedha kinachotumika kufadhili vita vya Urusi nchini Ukraine.

Majibu kutoka India

Wataalamu wanaamini kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Modi na Putin

Chanzo cha picha, Press Information Bureau (PIB)/Anadolu via Getty Images

Kiongozi wa upinzani Rahul Gandhi alimkosoa Waziri Mkuu Modi kwa kukubali kushinikizwa na Marekani. Alisema kauli za Trump zinaonyesha udhaifu wa msimamo wa Modi kuhusu Urusi.Haya ni kwa mujibu wa shirika la habari la PTI.

Kwa miezi kadhaa sasa, Modi amekuwa akisisitiza kwamba msimamo wa India katika vita vya Urusi na Ukraine ni wa kutoegemea upande wowote.

Hata hivyo, uhusiano wa kihistoria kati ya India na Urusi umeendelea kuwa imara.

Maafisa wa India wamekanusha madai kwamba nchi hiyo inanufaika na vita vya Urusi. Wamesema kuwa Marekani na Ulaya bado wanafanya biashara na Urusi licha ya vikwazo.

Mzozo wa mafuta wa Urusi umedhoofisha uhusiano kati ya Trump na Modi.

Licha ya tofauti hizo, Trump alimpongeza Modi Jumatano kwa kumuita “kiongozi mwenye maono.”

Modi naye alisema alizungumza na Trump wiki iliyopita, na walijadili maendeleo ya mazungumzo ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *