Manchester, England. Manchester United ina matumaini ya kupata ardhi zaidi ili kuharakisha mpango wao wa kujenga uwanja mpya wa kisasa utakaokuwa na uwezo wa kuingiza watu 100,000.
Bilionea na mmiliki mwenza wa Man United, Sir Jim Ratcliffe, aliweka wazi mpango wa kujenga uwanja Machi mwaka huu na kueleza kuwa utafunguliwa mwaka 2030.
Uwanja huo, unatarajiwa kutengenezwa kwa muundo wa paa kubwa la kipekee ambalo litaweza kufungwa na kufunguliwa pale inapohitajika kufanya hivyo.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayozuia kuanza kwa ujenzi wa uwanja huo ni eneo la kujengea ambalo linauzwa ghali mno na wamiliki.
Licha ya kwamba Man United inamiliki eneo la Old Trafford, bado inahitaji sehemu kubwa zaidi ili kujenga uwanja huo mpya.

Wiki iliyopita, jarida la SunSport liliripoti kuwa sehemu ya ardhi hiyo ambayo ipo karibu na Uwanja wa Old Trafford inayohitajika na Man United, inamilikiwa na bilionea mmoja kutoka Marseille.
Katika taarifa iliyotolewa na Man United kupitia tovuti yao na kurasa zao za mitandao ya kijamii, mashetani wekundu wamesema: “Ingawa tunamiliki sehemu kubwa ya ardhi inayozunguka Uwanja wa Old Trafford, kuna baadhi ya maeneo hatuyamiliki. Ili kufanikisha mradi wa uwanja mpya wa ukubwa huu, tunahitaji kuwa na eneo kubwa zaidi. Tumefanya mazungumzo na wamiliki wa ardhi wa maeneo hayo na tuna matumaini ya kufikia makubaliano katika miezi kadhaa ijayo.”
Sehemu nyingine ya ardhi ambayo Man United inataka kuinunua inamilikiwa na kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Freightliner.
Ripoti kutoka tovuti ya Daily Mail zinaeleza kuwa Man United imewasilisha ofa ya Pauni 50 milioni ili kulinunua lakini Freightliner inahitaji Pauni 400 milioni.

Hata hivyo, kwa sasa mazungumzo zaidi yanaendelea na huenda pande zote mbili zikafikia mwafaka na pengine kampuni hiyo ikakubali kuliuza eneo hilo kwa bei pungufu ya ile ambayo inahitaji sasa.