
Wakati wa tafakari na kujitolea upya
FAO ilianzishwa mwaka 1945 mara baada ya Vita Vikuu vya Pili yva Dunia ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula duniani, na sasa inatimiza miongo minane ya huduma. Kwa Bi. Tipo, ambaye pia anahudumu kama mwakilishi wa FAO nchini Kenya tangu Mei mwaka jana, hatua hii ni wakati wa kushukuru na pia wa kuchukua hatua.
“Huu ni wakati muhimu sana,” amesema. “Ni muda wa kutafakari tuliyoyafanikisha, kushukuru kwa ushirikiano wetu na serikali pamoja na washirika wa maendeleo, na kutoa wito wa kujitolea upya kufanikisha mifumo endelevu ya kilimo na chakula.”
Amesisitiza kuwa mafanikio ya FAO yamejengwa juu ya imani na ushirikiano na nchi wanachama. “Tumekuwa viongozi wa kimataifa katika kubadilisha mifumo ya kilimo na kukabiliana na migogoro kama vile milipuko ya magonjwa, huku tukibaki kuwa washirika wanaoaminika kwa nchi tunazozihudumia.”
Pamoja kwa Chakula Bora na Mustakabali Bora — Muktadha wa Tanzania
Kaulimbiu ya mwaka huu, “ Pamoja kwa Chakula Bora na Mustakabali Bora,” inaendana kwa karibu na hali ya Tanzania, ambako kilimo bado ni nguzo kuu ya maendeleo ya kitaifa. Bi. Tipo ametaja Dira ya Taifa ya mwaka 2050, ambapo FAO ni mshirika muhimu, anayesaidia kuendeleza mageuzi ya kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
“Tanzania tayari inajitosheleza kwa chakula,” ameeleza, “lakini bado kuna kazi ya kufanya ili kujenga mfumo wa chakula ulio imara na endelevu.” Hii ni pamoja na kuhakikisha chakula sio tu kinapatikana, bali pia ni salama, chenye lishe, na kinapatikana kwa bei nafuu kwa watu wote — hasa makundi yaliyo hatarini kama watoto, wanawake na wazee.
Kukabili changamoto kupitia ushirikiano
Licha ya maendeleo yaliyopatikana, Tanzania bado inakumbana na changamoto katika kubadilisha mifumo yake ya kilimo na chakula. Kwa mujibu wa Bi. Tipo, ambaye amekuwa akiongoza FAO nchini Tanzania tangu mwezi Desemba 2021, mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa zaidi.
“Tayari yanaathiri vibaya mifumo ya kilimo nchi nzima. Ndiyo maana tunafanya kazi kwa karibu na serikali kutekeleza mikakati ya kupunguza athari na kuhimili mabadiliko hayo,” ameeleza.
Mbali na tabianchi, vikwazo vingine muhimu ni ukosefu wa teknolojia za kisasa, pembejeo za kilimo, na huduma za kifedha — hasa vijijini. FAO, amesema, inashughulikia changamoto hizo kwa kufanya kazi “kwa kushirikiana bega kwa bega” na jamii, wizara za serikali, na sekta binafsi.
Mchango wa FAO Tanzania vijijini
Bi. Tipo ameeleza baadhi ya miradi ya FAO inayotoa matokeo dhahiri kwa wananchi:
- Kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi: Katika mikoa kama Kigoma, Dodoma, na visiwa vya Zanzibar, FAO inahamasisha mbinu za kilimo zinazoendana na mabadiliko ya tabianchi ili kulinda rutuba ya udongo na kuongeza mavuno endelevu.
- Mashamba darasa kwa wakulima: Programu hizi zinawawezesha wakulima kujifunza na kutumia teknolojia mpya, kama vile mbegu zinazostahimili ukame na zana za kidijitali za hali ya hewa ili kuboresha upangaji wa msimu wa kupanda na kuvuna.
- Kilimo kidijitali: Kuanzia ufuatiliaji wa magonjwa ya mimea hadi taarifa za magonjwa ya mifugo kupitia simu, suluhisho za kidijitali zinawasaidia wakulima kuongeza tija na kupunguza hatari.
- Uvuvi na mazingira: FAO pia inaunga mkono uvuvi endelevu kupitia mbinu zinazozingatia mifumo ya ikolojia, kwa lengo la kuhifadhi rasilimali za asili kwa vizazi vijavyo.
Mbali na miradi ya moja kwa moja, FAO inafanya kazi na serikali kuboresha sera, taasisi na mifumo ya usimamizi wa ubora wa chakula, maabara, na kanuni za udhibiti.
Ushirikishwaji wa wanawake na vijana: Kipaumbele cha mkakati
FAO inatambua nafasi muhimu ya wanawake na vijana katika kilimo, na kuhakikisha wanajumuishwa kikamilifu katika mipango yake nchini Tanzania.
“Zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa kilimo ni wanawake,” amesema Bi. Tipo. “Lakini teknolojia nyingi za kilimo hazikubuniwa kwa kuzingatia mahitaji ya wanawake. Ndiyo maana tunashirikiana na sekta binafsi kukuza teknolojia rafiki kwa wanawake na kuwawezesha kiuchumi.”
Miradi kama vile Mpango wa Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Wanawake Vijijini inalenga kuboresha upatikanaji wa fedha, masoko, na minyororo ya thamani kwa mazao wanayolima na kuchakata.
Kwa vijana, FAO inatumia uwezo wao wa teknolojia kuvutia kizazi kipya kwenye sekta ya kilimo kupitia ubunifu na kidijitali. “Kilimo kidijitali kinawavutia sana vijana,” ameongeza. “Ni njia muhimu ya kuwahusisha katika sekta hii.”
Mwelekeo wa siku za usoni
FAO inapoanza muongo wake wa tisa, ujumbe ni wazi: hatua za pamoja siyo tu kaulimbiu, bali ni hitaji la kweli. Nchini Tanzania na kwingineko, shirika linaendelea kutoa wito kwa wadau wote — serikali, jamii za kiraia, sekta binafsi, na jamii za wenyeji — kutembea kwa pamoja kuelekea mfumo wa chakula ulio sawa, thabiti na endelevu.
“FAO katika miaka 80 siyo sherehe tu,” amehitimisha Bi. Tipo. “Ni kujitolea upya kuwatumikia binadamu — na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika safari ya chakula bora na maisha bora.”