
Naibu Mkaguzi wa Kituo cha Kijeshi cha Khatam al-Anbiya amezungumzia makubaliano ya usitishaji vita kati ya HAMAS na utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa, makubaliano hayo yanatokana na Marekani na utawala wa Kizayuni kukata tamaa kwa sababu wamechoshwa mno na vita visivyo na mwisho licha ya jinai kubwa walizofanya Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Kamanda Asadi amesema hayo kwenye mahojiano maalumu aliyofanya usiku wa kuamkia leo Alkhamisi Oktoba 16 na huku akizungumzia uimara wa kambi ya Muqawama na wa taifa la Palestina amesema: Watu mashujaa wa Palestina wamepasi kishujaa na kwa uaminifu majaribio makubwa zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Amma kuhusu matamshi ya hivi karibuni ya rais wa Marekani, Kamanda Asadi amesema: Kwa kweli sijui watu wenye busara wanatazamaje kauli za hivi karibu za rais wa Marekani. Je, kuna uovu wowote ambao Trump hajafanya mpaka leo hii anajifanya anapenda amani? Je, kuna mabomu mazito zaidi… mauaji makubwa zaidi ya watoto, na uhalifu mbaya zaidi kuliko aliofanya Trump? Kwani hakushambulia mahospitali? Kwani hakuuwa waandishi wa habari na kushambulia magari ya wagonjwa? Nini kingine angeweza kufanya? Maneno haya ya kudai wamesimamisha vita kwa sababu wanapenda amani ni ya watu waliokata tamaa na kuona hawawezi kuufanya chochote Muqawama wa Palestina. Aidha amesema: “Walidai kuwa wanataka kuiangamiza Hamas. Je, Hamas imeangamizwa? Si tu HAMAS haijatoweka, lakini pia imeenea na kupata nguvu zaidi duniani kote.”
Akizungumzia historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, Kamanda Asadi amesema: “Wakati utawala wa kihalifu na muovu wa Pahlavi ulipokuwa kwenye kilele cha uwezo wake na ulipokuwa ukiwatupa wanafunzi kutoka kwenye ghorofa za Skuli ya Faiziyeh, Imam Khomeini (rehema za Allah na amani zimshukie) aliahidi kuporomoka utawala wa Shah lakini watu walimcheka. Matokeo yake utawala wa Pahlavi umeporomoka na njia hii ya mapambano inaendelea.
Akijibu swali kuhusu uwezekano wa Marekani na utawala wa Kizayuni kukanyaga makubaliano ya kusitisha vita Ghaza amesema: Makubaliano haya ya hivi sasa ni ya wakati ambao pande hizo mbili ziko vitani na zimekubaliana kusitisha vita. Swali muhimu hapa ni kwamba, hivi Hamas ina ndege au helikopta za kumzuia adui asishambulie? Haina. Lakini adui amelazimika kusimamisha vita. Hivyo makubaliano haya ni ya kukata tamaa upande wa Marekani na utawala wa Kizayuni, kwa sababu wamefanya jinai mpaka wamechoka na hawakupata chochote zaidi ya kuazirika tu duniani.