Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambao ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Kampala, mji mkuu wa Uganda kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).
Esmail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kupitia ujumbe aliotuma katika mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yuko Kampala, Uganda kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 19 wa kati ya muhula wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya NAM.
Mkutano wa 19 wa kati ya muhula wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote (NAM) umefanyika kwa siku mbili yaani jana Jumatano na leo Alhamisi huko Kampala mji mkuu wa Uganda. Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje na jumbe za ngazi ya juu kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya NAM.
Mbali na kushiriki katika majadiliano ya pamoja katika mkutano huo na kubainisha misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu matukio ya kimataifa, Araqchi pia amezungumza na kubadilishana mawazo na Mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje wa nchi zilizoshiriki katika mkutano huo.
Kuchunguza matukio ya kimataifa na kikanda kwa kutilia mkazo kanuni za nchi wanachama wa Jumuiya ya NAM, kuimarisha ushirikiano wa pande kadha miongoni mwa wanachama, na kubainisha wazi misimamo ya nchi mbalimbali kuhusu changamoto zinaoikabili dunia kama vile mabadiliko ya hali tabianchi, migogoro ya kibinadamu, kufanyiwa marekebisho miundo ya kimataifa, na matukio ya Gaza ni miongoni mwa mada muhimu zaidi zilizojadiliwa katika Mkutano wa Kampala.

Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote inazijumuisha nchi zaidi ya 120; jumuiya ambayo iliasisiwa wakati wa Vita Baridi. Iran ni kati ya wanachama muhimu na wenye taathira ndani ya jumuiya ya NAM ambayo ina nafasi muhimu katika kubuni sera za jumuiya hiyo khususan katika kukabiliana na sera na misimamo ya upande moja na kutetea uhuru wa nchi zinazoendelea duniani.
Mwaka 2012 Iran ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 16 wa jumuiya ya NAM mjini Tehran na ilikuwa mwenyekiti wa kiduru wa jumuiya ya NAM kwa muda wa miaka mitatu. Iran imekuwa ikitetea kanuni na misingi mikuu ya harakati hiyo, kama vile kutotegemea madola makubwa, kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya nchi nyingine na kukubaliana na vikwazo vya upande mmoja.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imenufaika na uwezo wa harakati hiyo katika kukabiliana na vikwazo vya Magharibi na imejaribu kuvutia hisia za nchi wanachama katika uwanja huo. Katiakkipindi chake kcha uwenyekiti wa kiduru wa jumuiya hiyo, Iran iliwasilisha mapendekezo kadha ili kufanyiwa marekebisho Mkatab wa Umoja wa Mataifa, kutekelezwa mageuzi katika suala la kupambana na ugaidi na kutekelezwa uadilifu katika mfumo wa uchumi wa dunia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeweza kuimarisha uhusiano kati yake na nchi za Kiafrika, za bara la Asia na Amerika ya Latini kupitia jumuiya ya NAM. Kufanyika mikutano na vikao vya kiutamaduni katika fremu ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote (NAM) kumeandaa uwanja wa kuarifishwa mitazamo ya Iran duniani.
Kufanyika Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya ya NAM huko Uganda ni fursa muhimu kwa ajili ya kushirikiana nchi huru duniani ili kuwahami, kuwatetea wananchi wa Palestina na kukabiliana na misimamo na hatua za upande mmoja duniani. Mgogoro wa kibinadamu huko Gaza umezipelekea nchi nyingi wanachama wa jumuiya hiyo kutoa wito wa kusimama kidete na kukabiliana na hatua za utawala wa Kizayuni. Katika mkutano wa Kampala, Kamati ya Palestina ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote imekutana ili kubainisha mshikamano na wananchi wa Palestina.
Kwa msingi huo, Mkutano wa Kampala ni fursa kwa nchi huru duniani kuwa na sauti ya pamoja ili kutetea haki na uhuru wa kisiasa dhidi ya udhibiti wa madola ya kibeberu duniani.