
Taasisi ya Israel ya Al-Sam, inayoshughulikia matibabu ya waraibu wa dawa za kulevya, imefichua katika taarifa yake kwamba asilimia 13 ya wanaopata matibabu ya uraibu katika taasisi hiyo ni askari wa akiba wa jeshi la Kizayuni.
Imesema, asilimia 18 ya wanajeshi waliohudumu katika operesheni inayoitwa “Upanga wa Chuma” ya utawala wa Kizayuni huko Gaza wanakabiliwa na matatizo ya uraibu. Taasisi hiyo imeendelea kusema kuwa askari wengi wa akiba wameonyesha kutoridhishwa na muda wao wa kuhudumu jeshini, huku wengine wakipoteza kazi zao au kulazimishwa talaka au kujitolea kwenye vituo vya wagonjwa wa akili, huku wengine wakigeukia bangi na dawa zingine za kulevya.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, athari za kisaikolojia na kijamii za vita vya Gaza zinazidi kujitokeza taratibu na kwamba jamii ya Israel inahitaji miaka na pengine miongo kadhaa ili kukabiliana na tatizo hilo.
Katika upande mwingine gazeti la Yemen la “Yemaniyun” limeandika kuwa, baada ya kupita takriban mwaka mmoja tangu yafikiwe makubaliano ya usitishaji vita kati ya Lebanon na utawala wa Kizayuni, uchokozi wa utawala huo kusini mwa nchi hiyo ungali unaendelea kwa uungaji mkono wa Marekani. Limeashiria kwamba raia mmoja wa Lebanon aliuawa shahidi katika shambulio la hivi karibuni la jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya gari la raia katika eneo la Sour na kuongeza: ‘Uchokozi huu wa utawala wa Israel unafanyika huku Umoja wa Mataifa ukidai kuwepo eti “utulivu mkubwa” katika mipaka ya Lebanon, suala ambalo ukweli wa mambo unaonyesha kinyume hake.’