Picha ya karibu ya Kanali Michael Randrianirina. Amevaa sare za kijeshi.

    • Author, Wedaeli Chibelushi
    • Nafasi,
    • Author, Omega Rakotomalala
    • Nafasi, BBC Monitoring
    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, BBC Africa

Kabla ya mwisho wa wiki iliyopita, jina la Kanali Michael Randrianirina halikujulikana sana nchini Madagascar. Ungewaulizia watu kumhusu, wangekutazama bila majibu.

Lakini ndani ya siku tatu, amegeuka kuwa mtu mwenye mamlaka ya juu zaidi nchini humo.

Jumamosi, akiwa mkuu wa kikosi maalum cha jeshi cha CAPSAT, Randrianirina aliingia katikati ya mji mkuu Antananarivo na wanajeshi wake, na kuungana na waandamanaji waliokuwa wakimtaka Rais Andry Rajoelina ajiuzulu.

Baada ya Rajoelina kuondoka jijini na Bunge kupiga kura ya kumuondoa madarakani, Randrianirina, mwenye umri wa miaka 51, alisimama mbele ya ikulu iliyoachwa wazi na kutangaza kuwa CAPSAT imechukua mamlaka.

Mahakama ya Katiba baadaye ilimtangaza kuwa mtawala mpya wa nchi, ingawa Rajoelina bado anadai kuwa yeye ndiye rais halali.

Randrianirina hajulikani sana hadharani, licha ya kuwa ameongoza kikosi chenye ushawishi mkubwa jeshini.

Alizaliwa katika kijiji cha Sevohipoty, mkoa wa Androy kusini mwa Madagascar.

Miaka ya 2016 hadi 2018, alihudumu kama gavana wa Androy chini ya Rais wa zamani Hery Rajaonarimampianina, kisha akaongoza kikosi cha askari wa miguu mjini Toliara hadi 2022.

Alikuwa mkosoaji wa wazi wa Rajoelina, mfanyabiashara aliyepindua serikali mwaka 2009, akaondoka 2013 na kurejea madarakani baada ya uchaguzi wa 2018.

Mwaka 2023, Randrianirina alikamatwa na kuwekwa katika gereza la ulinzi mkali bila kufikishwa mahakamani, akituhumiwa kupanga mapinduzi na kuchochea uasi.

Aliachiwa huru Februari 2024 baada ya shinikizo kutoka kwa wanajeshi, wanafunzi na wanasiasa waliodai alifungwa kwa misingi ya kisiasa.

Saa chache kabla ya kutangaza rasmi kuchukua mamlaka, Randrianirina aliambia BBC kuwa yeye ni “mtumishi wa wananchi.” Alizungumza kwa utulivu na bila kujifahari.

Mwandishi wa Madagascar, Rivonala Razafison, anamweleza kama mtu ”nyoofu”, ”mwenye msimamo thabiti” na ”mzalendo”.

G

Chanzo cha picha, Getty Images

Randrianirina amekosoa kwa uwazi ushawishi wa Ufaransa, nchi iliyotawala Madagascar hadi mwaka 1960.

Alipopewa fursa ya kujibu maswali ya BBC kwa Kifaransa, alikataa: “Kwa nini nisiweze kuzungumza lugha yangu, Kimalagasi?” Randrianirina aliuliza? na kuongeza kuwa hapendi kutukuza lugha ya kikoloni.

Kiongozi huyo wa CAPSAT ameambia vyombo vya habari kuwa kipaumbele chake ni ”ustawi wa jamii”, hasa katika nchi ambayo karibu asilimia 75 ya watu wanaishi katika umaskini.

Ameeleza kuwa jeshi litaongoza kwa kipindi cha hadi miaka miwili sambamba na serikali ya kiraia, kabla ya uchaguzi kuandaliwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya shirika la Reuters, Randrianirina anatarajiwa kuapishwa katika siku moja au mbili zijazo. Hii itakuwa hitimisho la siku chache za mageuzi makubwa yaliyomuinua kutoka gerezani hadi ikulu.

Soma pia:

Hisia mseto kufuatia mapinduzi ya Madagascar

G

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Kiongozi wa kijeshi Kanali Michael Randrianirina ataapishwa kama rais wa mpito wa Madagascar siku ya Ijumaa, uongozi mpya wa nchi hiyo umetangaza, huku Umoja wa Afrika (AU) ukisema utawaekea vikwazo nchi hiyo baada ya mapinduzi ya kumuondoa rais Andry Rajoelina.

Kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa ulisema “una wasiwasi mkubwa na mabadiliko ya mamlaka kinyume na katiba”.

Ufaransa ilisema katika taarifa yake kwamba “ni muhimu kwamba demokrasia, uhuru wa kimsingi, na utawala wa sheria udumishwe kwa uangalifu”.

Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani alisema wahusika wote wanahitajika “kuchukua hatua kwa tahadhari katika hali hii ya kutatanisha kwa sasa”, huku Urusi ikitoa wito wa “kujizuia na kuzuia umwagaji damu”.

Isitoshe, Bodi ya usalama ya kambi ya SADC ya kikanda – ambayo Rajoelina alikuwa akishikilia urais wa zamu – pia ilionyesha wasiwasi.

Mji mkuu, Antananarivo, unasalia tulivu mwishoni mwa Jumatano, ingawa kuna kutokuwa na uhakika ni kipi kinaweza kutokea baadaye.

Wakati huo huo, Tamasha lilifanyika kwenye uwanja wa Symbolic Place du 13 Mai, mbele ya ukumbi wa jiji, ambapo maelfu ya waandamanaji na magari yaliyokuwa na silaha yalikuwa yamepigana siku zilizopita.

Taifa hilo la Bahari ya Hindi limetumbukia katika msukosuko mbaya zaidi wa kisiasa kuwahi kutokea kwa miaka kadhaa baada ya kikosi cha wasomi cha CAPSAT kuchukua madaraka siku ya Jumanne, muda mfupi baada ya bunge kupiga kura ya kumshtaki Rajoelina, ambaye alionekana kuikimbia nchi wakati maandamano ya mitaani yakiongezeka.

Limekuwa koloni la hivi punde zaidi la Ufaransa kuwa chini ya udhibiti wa kijeshi tangu 2020, baada ya mapinduzi katika Mali, Burkina Faso, Niger, Gabon na Guinea.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *