Siku ya Chakula Duniani leo hii, tarehe 16 Oktoba, hapa kuna mambo matano unayopaswa kuyajua kuhusu jinsi ya kuwalisha watu zaidi ya bilioni nane duniani.

1. Mizozo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa

Mizozo ya silaha, kama ile inayoendelea huko Ukraine, Sudan na Gaza, huathiri uzalishaji wa chakula, minyororo ya usambazaji, na upatikanaji wa masoko, na kusababisha watu kuhama makazi, jambo linalosababisha njaa kali kwa mamilioni ya watu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa  Haití, takriban watu milioni 5.7 wanakabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula, ambapo watu milioni 1.9 wako kwenye hali ya dharura.

WFP inasambaza chakula kinachohitajika sana kwa wakazi wa Cité Soleil, Haiti.

© WFP/Tanya Birkbeck

WFP inasambaza chakula kinachohitajika sana kwa wakazi wa Cité Soleil, Haiti.

Katika maeneo yenye mizozo, Umoja wa Mataifa, hasa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la  Mpango wa Chakula Duniani (WFP), hutoa msaada wa chakula kwa watu wanaokabiliwa na njaa kali. Jamii zinazohusika pia hupatiwa mbegu, mifugo na zana za kilimo ili waweze kujilisha wenyewe na wasitegemee msaada tu.

2. Mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa

Mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko na joto kali, huathiri sana uwezo wa wakulima kuzalisha chakula. Hii hupunguza uzalishaji wa kilimo na upatikanaji wa chakula, hasa katika maeneo hatarishi.

Nchi kama Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Mali, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria na Ethiopia zinakabiliwa na njaa kali inayosababishwa na mizozo, mafuriko na ukame. Somalia kwa mfano, inakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miongo minne, hali inayoongeza mateso yanayotokana na mizozo na watu kufurushwa makwao.

Mvulana akisukuma chombo cha maji huko Dollow kwenye mpaka wa Somalia na Ethiopia.

© UNICEF/Zerihun Sewunet

Mvulana akisukuma chombo cha maji huko Dollow kwenye mpaka wa Somalia na Ethiopia.

Umoja wa Mataifa unapendekeza mbinu za kilimo zenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ili kupunguza athari za mazingira na kuendana na mabadiliko haya, kama vile mbinu ya kilimo ijulikanayo kama “half-moon” katika Ukanda wa Sahel barani Afrika.

3. Mgogoro wa kiuchumi na mfumuko wa bei

Mgogoro wa kiuchumi duniani na ya kikanda, kupanda kwa bei ya chakula na nishati, na mfumuko wa bei vimepunguza uwezo wa watu kununua chakula bora, hasa katika nchi maskini.

Janga la coronavirus“>COVID-19, vita vya Ukraine na mabadiliko ya tabianchi vilichangia kuongezeka kwa bei ya chakula kati ya 2020 na 2024. Bei za chakula zilipozidi kuongezeka, mishahara halisi ilishuka na mfumuko wa bei ukaongezeka, watu hasa katika nchi maskini ulipungua uwezo wao wa kununua chakula bora na mara nyingi walipunguza idadi ya milo wanayokula kwa siku.

Msichana mwenye umri wa miaka miwili anakula chakula chenye virutubisho katika kituo cha afya huko Maiduguri kaskazini mwa Nigeria.

© WFP/Arete/Damilola Onafuwa

Msichana mwenye umri wa miaka miwili anakula chakula chenye virutubisho katika kituo cha afya huko Maiduguri kaskazini mwa Nigeria.

Katika nyakati za mgogoro wa kiuchumi na mfumuko wa bei, Umoja wa Mataifa huongeza usambazaji wa chakula na virutubisho pamoja na kutoa misaada ya fedha ili kusaidia familia kununua chakula wao wenyewe, na hivyo kusaidia lishe na masoko ya ndani.

4.  Umasikini wa kimuundo na ukosefu wa usawa

Umasikini wa kina na ukosefu wa usawa huzuia upatikanaji wa chakula na rasilimali, hasa katika jamii za vijijini na za pembezoni, na hivyo kuendelea kuwepo kwa njaa sugu.

Mapato madogo, miundombinu duni na huduma za chini mara nyingi husababisha watu katika jamii za pembezoni hasa wanawake na makundi ya jamii za watu wa asili kushindwa kupata chakula cha kutosha.

Takriban watu milioni 700 wanaishi katika umasikini mkubwa duniani, ambapo takriban theluthi mbili wapo katika  Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake unajaribu kuimarisha mifumo ya ulinzi wa hifadhi ya jamii na kuhamia kutoka misaada ya dharura kuelekea mfumo unaowawezesha nchi masikini kujenga mifumo ya chakula yenye ustawi, usawa na inayohimili mabadiliko.

Njia hii huwasaidia jamii kupunguza njaa, kujijengea uwezo wa ndani na kuboresha usalama wa chakula kwa muda mrefu.

5. Mizunguko ya biashara na mabadiliko ya bei za masokoni

Vikwazo vya kuuza bidhaa nje, ushuru, na mabadiliko yasiyotabirika ya bei za bidhaa huleta mizunguko isiyo thabiti ya masoko ya chakula, na kuufanya chakula kuwa kigumu kupatikana na cha gharama kubwa katika nchi zinazotegemea chakula kutoka nje.

Nchini Bangladesh, wakulima wanapanda mimea inayostahimili hali ya hewa.

© IFAD/GMB Akash

Nchini Bangladesh, wakulima wanapanda mimea inayostahimili hali ya hewa.

Bangladesh, Pakistan, na Sri Lanka zinakabiliana na mabadiliko ya bei ya chakula na changamoto za madeni. Hali hizi zinazidi kuongezeka kutokana na kutokuwa na uhakika wa sera za biashara, hasa ushuru wa dunia na mfumuko wa bei. Hii mwishowe inazuia watu kupata chakula cha gharama nafuu.

Brazil na Mexico zimepata changamoto ya ukuaji wa uchumi kutokana na mvutano wa biashara na mfumuko wa bei, jambo ambalo limeongeza ukosefu wa chakula miongoni mwa watu wa kipato cha chini.

Moja wa Mataifa unafanya kazi kwa njia mbalimbali kusaidia nchi zinazokabiliwa na changamoto hizi. Unafuatilia bei za kimataifa, kutoa miongozo ya sera, na kuratibu hatua za kimataifa kusaidia nchi kushughulikia changamoto za chakula, nishati na fedha. Juhudi hizi zinalenga kuimarisha masoko na kulinda watu walio hatarini.

Siku ya Chakula Duniani inalenga kutambua na kusisitiza kwamba kila mtu, popote pale alipo duniani, anapaswa kupata chakula cha kutosha.

Kwa sasa, takriban watu milioni 673 wanateseka na njaa.

Wakati vita vinaendelea na mabadiliko ya tabianchi yanaathiri uzalishaji wa chakula, jumuiya ya kimataifa imeaomba ushirikiano wa pamoja wa dunia kuunda mustakabali wenye uhakika wa chakula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *