Tanga. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kiwango cha wananchi kuugua magonjwa yasiyoambuliza nchini Tanzania kinazidi kuongezeka na kuwataka kujenga tabia ya kula kwa mpangilio unaoshauriwa kiafya.

Amewakata kutokula kila chakula Ili kujikinga na magonjwa yasiyoambuliza yakiwamo ya kisukari na presha.

Ametoa wito huo leo Alhamisi Oktoba 16,2025 alipokuwa akifunga maadhimisho ya 45 ya siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Tanga.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua bidhaa mbalimbali wakati wa kilele cha maadhimisho ya 45 ya siku ya chakula Duniani yaliyofanyika kitaifa Jijini Tanga

“Ongezeko la unene kwa watoto na watu wazima limekuwa kubwa. Unene uliopitiliza siyo afya ,tusile kila kitu…tule kwa kufuata kanuni za kiafya lakini tufanye mazoezi,”amesema Majaliwa.

Kuhusu suala la lishe kitaifa Waziri Mkuu amesema limeendelea kuimarika kutokata uzalishaji wa mazao ya chakula kuongezeka.

“Serikali imeitengea Wizara ya Kilimo Sh1.3 trilioni mwaka huu wa fedha kutoka Sh246 bilioni, lengo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara Ili Tanzania iweze kuwa kinara wa mazao ya kilimo,”amesema Majaliwa.

Kwa upande wa ufugaji amesema ng’ombe wamefikia milioni 39.2 na kuku milioni 108 huku maziwa yakizalishwa lita 3.97 bilioni.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua bidhaa mbalimbali wakati wa kilele cha maadhimisho ya 45 ya siku ya chakula Duniani yaliyofanyika kitaifa Jijini Tanga

Kuhusu uvuvi, Waziri Mkuu amesema uzalishaji wa samaki umeongezeka kutokana na Serikali kugawa kwa wavuvi boti za kisasa huku ikitoa elimu ya ufugaji kwa kutumia vizimba.

“Serikali imefanya maamuzi ya kutenga bajeti ya kutosha katika wizara za kisekta ili kuimarisha kilimo, uvuvi na ufugaji kwa lengo la kuongeza mazao ya chakula kwa ajili ya kuboresha lishe kwa wananchi,”amesema Majaliwa.

Amewataka wakulima kutumia msimu ujao wa kilimo kwa kutayarisha mashamba mapema ili kuwahi mvua zitakapoanza kunyesha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Jerald Mweri amesema tayari Serikali imetenga tani 970,000 za mbolea ya ruzuku kwa ajili ya kugawa kwa wakulima wa mikoa mbalimbali nchini.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kwa upande wa mbegu za mahindi amesema wizara hiyo imetenga tani 10,000 kwa ajili ya kugawa kwa wakulima wa zao hilo waliopo mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

“Lengo ni kutekeleza kwa vitendo dira ya Taifa inayoelekeza Tanzania kujitosheleza kwa chakula.”

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi  Batilda Burian amesema jumla ya waoneshaji 578 wa bidhaa mbalimbali za kilimo na chakula wameshiriki katika mabanda ya maonyesho yaliyowekwa katika uwanja wa Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo kitaifa yaliyozinduliwa Oktoba 10 mwaka huu.
“Upatikanaji wa mitaji, kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa watoto na wanafunzi, umhimu wa lishe katika kudhibiti udumavu pamoja na mjadala wa kumbukizi ya Mwalimu Nyerere vilikuwa sehemu ya maadhimisho haya,”amesema Burian.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *