Moshi. Mgombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara ameahidi endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, atafanya mageuzi ya kiuchumi na kijamii kupitia nguzo kuu tatu za Kilimo, Viwanda na Teknolojia.

Amesema chama chake kinalenga kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania na kujenga kesho bora kwa vizazi vijavyo.

Kyara ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika uwanja wa Manyema, Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Mgombea huyo amesema utafiti uliofanywa na chama hicho umebaini kupitia nguzo hizo tatu, Tanzania inaweza kusonga mbele kiuchumi, kupunguza ukosefu wa ajira, na kuimarisha afya za wananchi.

Katika Kilimo, Kyara amesema atahamasisha kilimo hai lengo likiwa ni kuwezesha watanzania kula chakula bora kisicho na kemikali na kuingia kwenye ushindani wa soko la bidhaa na vyakula visivyo na kemikali ambalo ni kubwa kwa sasa duniani.

“Tumejipanga kuhimiza kilimo hai kwa Watanzania. Tafiti zinaonyesha kuwa watu wengi sasa wanakimbilia kula vyakula visivyo na kemikali kwa kuwa wanajua vinaimarisha afya na kusaidia kuzalisha kizazi chenye nguvu na kinga bora dhidi ya magonjwa,” amesema Kyara.

Ameongeza kwa sasa ni kawaida kusikia watoto wachanga wamezaliwa wakiwa na  magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, presha na magonjwa ya moyo yanayotokana na vitu walivyotumia wazazi wakati wa ujauzito.

“Tunahitaji kuzungumza na Watanzania kuhusu fursa kubwa iliyopo duniani ya bidhaa asilia zisizo na kemikali. Soko lake ni kubwa na linaweza kuongeza kipato cha wakulima wetu,” amesisitiza mgombea huyo.

Aidha, amegusia tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, akisema mfumo wa elimu wa sasa hauendani na mahitaji ya soko la ajira.

“Vijana wengi wanamaliza shule na vyuo bila ujuzi wa kufanya kazi za uzalishaji. Kama hajafundishwa kulima au kujiajiri, anakosa cha kufanya. Hivyo tunataka kubadilisha mfumo huu na kuweka elimu yenye tija na matokeo,” amesema.

Kyara amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura na kuichagua SAU ili kujenga taifa lenye maadili, uadilifu na uzalendo.

“Muda wa Mungu wa kuikomboa nchi yetu na kuitafutia mafanikio Tanzania ni mwaka huu 2025. Ni wajibu wetu kwenda kufanya maamuzi sahihi kupitia sanduku la kura,” amesema.

Kyara ametumia mkutano huo  pia kutoa salamu za pole kwa wananchi wa Kenya kufuatia kifo cha Waziri Mkuu mstaafu na kiongozi mashuhuri wa taifa hilo, Raila Odinga.

“Wenzetu wamepoteza jembe, mtetezi wa katiba yao. Ni pigo kubwa kwa Afrika Mashariki,” amesema Kyara.

Naye mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia chama hicho, Isaack Kireti amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo ataufanya mji wa Moshi kuwa wa matunda kwa kupanda miti mingi zaidi lengo likiwa ni kuimarisha afya za wananchi.

“Nipeni nafasi ya kuwa mbunge wa Moshi mjini nikaufanye mji huu kuwa na matunda kila eneo. Nataka iitwe Moshi ya matunda. Lakini pia nitahakikisha barabara zinapanuliwa ili kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa tishio” amesema na kuongeza;

“Lakini pia lipo soko la mitumba Memorial, nitahakikisha wananchi wanaoenda katika soko hilo wanapelekwa na kurejeshwa na magari atakayoyatenga bila malipo ili kukuza biashara za wajasiriamali walioko katika soko hilo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *