
WAKATI wa dirisha kubwa la usajili, tuliona na kushuhudia sana tambo katika timu mbili kubwa za Yanga na Simba kwa wachezaji wao wapya ambao ziliwasajili.
Sisi kijiweni kwa vile ni watu wa mpira, tukasema ngoja tujipe muda kabla ya kusifia kama wanavyofanya wengine maana tulijua muda ndio utakuwa hakimu sahihi.
Tuliamua kuziacha tambo kwa wenye mamlaka ya kuzisemea timu hizo na wale wachambuzi wa mihemko ambao wao huwa wanaamua kusifia tu au kuponda ilimradi kitu kimefanywa na mojawapo kati ya timu hizo mbili za Kariakoo.
Kijiwe kilifikia muafaka kwamba tathmini ianze kufanywa baada ya mechi kadhaa za msimu huu na sio kama ilivyokuwa inafanyika kwa wengine kabla hata msimu haujaanza kisa tu wengi wao wameona vipande vya video huko YouTube.
Sasa basi kwa vile Simba na Yanga zimeshacheza angalau mechi zisizopungua tano za mashindano katika msimu huu, leo kijiwe kinaanza kutoa tathmini yake ya wachezaji ambao timu hizo hazijakosea kuwasajili.
Kwa Yanga kijiwe kinakoshwa sana na yule Mohamed Doumbia, raia wa Ivory Coast, anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji. Jamaa ana jicho la pasi, anaweza kumiliki boli na kupiga pasi za maelekezo.
Pale Simba kuna yule beki Rushine De Reuck ambaye timu hiyo imemsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Beki mzuri, anajua kukaba, makadirio yake anapokabiliana na mchezaji wa timu pinzani ni sahihi na pia ana utulivu na matumizi mazuri ya akili.
Ndani ya muda mfupi, hao wachezaji nadhani wameshaonyesha kwa nini timu zao zilikubali kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwaleta nchini ili wazitumikie.
Kuhusu wachezaji wengine, naomba nitunze akiba ya maneno na kuendelea kuwapa muda kidogo. Mpira ni mchezo wa ajabu, wasije kuniumbua.