KIUKWELI hakuna anayefurahia kuona Taifa Stars haifanyi vizuri katika mashindano ambayo imekuwa ikishiriki mfano ni hayo ya kuwania Kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.

Tunatamani kuona timu yetu inatamba hata kama sio kwa daraja la juu sana lakini katika namna ambayo itafanya timu pinzani zisituchukulie poa na ziwe angalau na hofu kidogo zinapokutana na sisi katika mashindano tofauti.

Lakini kwa sasa ni tofauti, Taifa Stars haina makali hayo ya kufanya timu sio tu zile kubwa bali hata zile za saizi yetu kutuhofia na badala yake zinaona zinaweza kupata matokeo mazuri dhidi yetu.

Mfano hivi sasa, Taifa Stars imeshindwa angalau kumaliza hata katika nafasi ya pili kwenye kundi lake la kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani na haijafikisha angalau pointi 10 katika kundi hilo ambalo lilikuwa na Zambia ambayo haijacheza vizuri na Niger iliyo katika daraja la kati.

Sasa kuna njia tatu ambazo kijiwe kinaamini mojawapo inaweza kuwa msaada kwa Taifa Stars na kufanya siku moja iwe kati ya timu tishio barani Afrika na isiwe mnyonge dhidi ya timu bora.

Njia ya kwanza ni kuwa na wachezaji bora wazawa wanaocheza soka katika ligi yetu. Wenye darajala ubora wa kushindana kimataifa. Hapa tutakuwa kama Afrika Kusini ambayo imebebwa na wachezaji wa namna hiyo.

Kama tukishindwa njia hiyo, basi tujitahidi kupeleka kundi kubwa la wachezaji wetu kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya bara la Afrika hasa huko Ulaya katika ligi ambazo zitawafanya waimarike zaidi. Njia hii ndio inazibeba timu kama Ivory Coast, Senegal, Ghana na kadhalika.

Halafu kuna njia ya tatu ambayo ni kutafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza soka la kulipwa huko Ulaya na kisha kuwatumia katika timu yetu ya taifa. Cape Verde ambayo imefuzu kwa mara ya kwanza Fainali za Kombe la Dunia 2026, inatumia njia hii.

Kupanga ni kuchagua. Tunaweza kuamua kufuata njia zote, njia mojawapo au kuziacha zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *