
Dar es Salaam. Kwa wasio na ajira na waliosomea taaluma hizi, huu ni wakati muafaka wa kuchangamkia fursa za ajira zilizotangazwa na Serikali. Nafasi 17,710 za ajira kwa taasisi na mamlaka za Serikali zipo tayari kuwaniwa kwa watakaokidhi vigezo na wenye sifa stahiki.
Kwa mujibu wa tangazo la ajira lililotolewa leo, Alhamisi Oktoba 16, 2025, linatoa fursa kwa Watanzania wenye sifa na uwezo kuchangamkia ajira hizo, lengo likiwa ni kuimarisha utoaji wa huduma kwa umma na kuboresha ufanisi.
Miongoni mwa kada zenye nafasi nyingi ni ofisa muuguzi msaidizi (3,945), dereva daraja la II (427), ofisa kilimo msaidizi (292), ofisa mifugo msaidizi (252) na ofisa hesabu daraja la II (224).
Pia zipo nafasi kwa wahasibu, wataalamu wa Tehama, wataalamu wa afya ya mazingira, maendeleo ya jamii, ushirika, uvuvi, uhandisi, ustawi wa jamii, michezo, utamaduni, malezi ya watoto pamoja na wataalamu wa mifumo ya fedha.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, kila nafasi imeainishwa majukumu, sifa za mwombaji na ngazi ya mshahara kulingana na viwango vya Serikali (TGS na TGHS).
Kwa mfano, nafasi za wahasibu daraja la II zinahitaji wahitimu wa Shahada ya Uhasibu au Biashara waliopata CPA (T) au sifa zinazofanana, huku nafasi za wasaidizi wa hesabu zikihitaji wahitimu wa Astashahada ya Uhasibu.
Katika sekta ya kilimo na uvuvi, Serikali inatafuta maofisa kilimo, uvuvi na ufugaji nyuki kwa lengo la kuimarisha uzalishaji, kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji, pamoja na kukuza sekta ya chakula na lishe.
Vilevile, nafasi za wahandisi wa kilimo na mazingira zinalenga kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na usimamizi endelevu wa mazingira.
Sekta ya afya imepewa kipaumbele kikubwa, kwani zaidi ya nusu ya nafasi zimetengwa kwa kada hiyo, ikiwemo wauguzi, madaktari wa kinywa na meno, wataalamu wa afya ya mazingira na wahandisi wa vifaatiba.
Hatua hii inalenga kupunguza uhaba wa watumishi katika hospitali na vituo vya afya vya wilaya na vijiji kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa utawala na usimamizi, nafasi zimefunguliwa kwa maofisa utawala, wachumi, maofisa sheria, maofisa ununuzi, wahasibu na maofisa maendeleo ya jamii, ambao watasaidia kuboresha uwajibikaji na utendaji serikalini katika kutoa huduma kwa wananchi.
Watanzania wanaotaka kuomba wanatakiwa kuwa na sifa zinazotambuliwa na Serikali na vyuo husika, pamoja na ujuzi wa kutumia kompyuta kwa kada nyingi.
Waombaji wote wanapaswa kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo wa kielektroniki wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kupitia tovuti ya www.ajira.go.tz ndani ya muda uliopangwa.
Tangazo hilo limeainisha viwango vya mishahara kulingana na kada, kuanzia TGS.B hadi TGS.E na TGHS kwa kada za afya.
Pia limeeleza kuwa waombaji waliowahi kuomba nafasi serikalini hawana kizuizi cha kuomba tena endapo wanakidhi vigezo vilivyowekwa.
Serikali imesema ajira hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuongeza watumishi katika sekta muhimu za uchumi na huduma za jamii, sambamba na dhamira ya kuhakikisha huduma za afya, elimu, kilimo na miundombinu zinaboreshwa nchini kote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nafasi hizo zimeandaliwa kwa uwiano unaozingatia mahitaji ya kila sekta, uwiano wa kijinsia na usawa wa kikanda.
Waombaji wametakiwa kusoma kwa makini maelekezo ya tangazo, kuambatanisha vyeti sahihi vilivyohakikiwa, na kuepuka kuwasilisha maombi yenye upotoshaji au nyaraka feki.