London, England. Sheria mpya ya ukomo wa mishahara kwa Ligi Kuu England inayopendekezwa ambayo baadhi ya timu hazitaki kabisa, inaweza kuanza kutumika mapema mwezi ujao.
Klabu za EPL zinatarajiwa kupiga kura kuhusu mfumo unaoitwa ‘anchoring’, ikiwa na maana ya mwongozo ambao utaweka ukomo wa matumizi ya mshahara kwa kila timu kwa kuzingatia kiasi cha pesa ambacho timu ya mwisho katika msimamo imekipata.
Klabu za Manchester City na Manchester United zinapinga mfumo huu, zikisema utapunguza ubora wa Ligi Kuu England na kuwafanya wachezaji bora duniani kuondoka kwenda ligi nyingine kama La Liga na Bundesliga. Wengine wanasema utafanya iwe ngumu zaidi kwa timu zinazopanda daraja kuhimili ushindani wa Ligi Kuu.
Mwongozo huu, unaoitwa ‘top to bottom anchor’, utamaanisha klabu haziwezi kutumia zaidi ya mara tano ya mapato ya timu iliyomaliza nafasi ya mwisho.

Matumizi hayo yatahusisha gharama zote za usajili wa wachezaji, benchi la ufundi, mishahara na ada za mawakala.
Hiyo ina maana ikiwa msimu uliopita timu ya mwisho katika msimamo iliingiza Pauni 100 milioni kutokana na pesa za haki ya matangazo ya televisheni na bonasi nyingine, hakuna timu ambayo ingeruhusiwa kuvuka matumizi ya Pauni 500 milioni katika matumizi yao ya dirisha hili.
Katika mapendekezo hayo ambayo yameandaliwa na Chama Cha Soka cha England, yanaeleza timu ambayo itakiuka sheria hiyo mara mbili baada ya kupitishwa basi itapokonywa pointi sita na pointi moja ya ziada kwa kila Pauni 6.5 milioni zitakazozidi.
Wakosoaji wanasema mfumo huu utazuia klabu za England kulipa mishahara mikubwa kama ya klabu za Ulaya ambazo havitafungwa na sheria hii, jambo ambalo linaweza kuwafanya wachezaji kama Erling Haaland na Mohamed Salah kuhamia timu kama Real Madrid, Barcelona, au Bayern Munich.
Vilevile kuna hofu kubwa wachezaji wengi kutoka ligi hiyo wanaweza kutimkia Saudi Arabia.
Sir Jim Ratcliffe, mmiliki mwenza wa Manchester United, amesema: “Mfumo huu utadhoofisha klabu kubwa za EPL. Hatutaki kuona klabu zetu zikiwa haziwezi kushindana na Real Madrid au PSG, hili jambo halina maana. Tukiruhusu hilo EPL haitaendelea kuwa ligi bora duniani.”

Wadau wengine wanaopinga mfumo huu wanasema ukipitishwa utapunguza hamasa ya klabu kuwekeza zaidi na baadhi ya wamiliki wanaweza kunufaika kifedha kwa muda mfupi kwa sababu watapunguza matumizi.
Kwa sasa, klabu zitapiga kura katika wiki chache zijazo na matokeo yake yanaweza kubadilisha kabisa mfumo wa kifedha wa soka la England.