
Shirika la kutetea haki za binadamu la Mashad limerekodi vifo vya raia 146, wakiwemo watoto 41 katika siku za hivi karibuni katika mji El-Fasher magharibi mwa Sudan.
Shirika hilo la kufuatilia matukio ya Sudan limezitaja hatua na mashambulizi ya RSF kama “ukatili wa kimfumo unaojumuisha uhalifu wa kivita, likitaja tukio la kushambuliwa kwa makombora kwa makusudi katika maeneo ya makazi na kunyongwa kwa wale waliokimbia ghasia.
Nayo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetahadharisha kuhusu matokeo mabaya kama mzingiro utaendelea, ikiashiria uhaba mkubwa wa chakula, miripuko ya magonjwa, na kukaribia kuporomoka kwa huduma za afya.
“El Fasher, Darfur Kaskazini, inaendelea kuzingirwa,” OCHA imesema katika ujumbe kwenye X jana Jumatano. “Zaidi ya raia 260,000, nusu yao wakiwa watoto, wamenaswa katikati ya mashambulizi yasiyokoma, njaa na kipindupindu.”
Haya yanajiri siku chache baada ya Jeshi la Sudan (SAF) kudai kuwa, zaidi ya wapiganaji 100 wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) wameuawa katika mapigano ya El-Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini huko magharibi mwa Sudan.
Jumamosi iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilidai pia kwamba mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za RSF yaliua raia 57 katika makazi ya muda ya wakimbizi wa ndani huko El-Fasher. Hata hivyo, siku iliyofuata yaani siku ya Jumapili RSF ilikanusha vikali kuhusika na shambulio hilo.
Mapigano makali yamekuwa yakiendelea huko El-Fasher tangu Mei 2024, kati ya SAF na vikosi vya washirika kwa upande mmoja na RSF kwa upande mwingine, huku mapigano yakizidi katika siku za hivi karibuni.