Tottenham Hotspur inadaiwa kuwa katika mipango mikubwa ya kumsajili straika wa Bayern Munich, Harry Kane dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwakani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Teamtalk, Spurs ipo tayari kulipa kiasi kinachohitajika ili kuvunja mkataba wake na pia ipo tayari kulipa mshahara sawa na ule anaolipwa sasa akiwa na Bayern.

Kane, 31, alijiunga na Bayern mwaka 2023 kwa ada ya takribani Pauni 100 milioni akitokea Spurs na hadi sasa amefunga mabao 103 katika mechi 106 za michuano yote alizocheza akiwa na jezi ya timu hiyo.

Hata hivyo, hivi karibuni Kane mwenyewe alipoulizwa ikiwa anaweza akaondoka, alisema hafikirii hilo kwa sasa kwani anajisikia furaha na kila kitu kipo sawa.

Ripoti pia zinaonyesha kitu pekee kinachoweza kumfanya staa huyu arejee London ni kutaka kuwa karibu na familia yake kwa sababu licha ya kuishi nayo jijini Munich kwa muda, mara nyingi watoto na mkewe huwa London ambako kuna nyumba yao.

Elliot Anderson

MANCHESTER City inajiandaa kutoa ofa ya Pauni 75 milioni kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Nottingham Forest, Elliot Anderson dirisha lijalo la majira ya baridi. Hata hivyo, matajiri hao wa Jiji la Manchester wanatarajiwa kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Chelsea, ambao pia wanamfuatilia kwa karibu mchezaji huyo, 22. Kwa mujibu wa gazeti la The Express, Pep Guardiola anataka kuimarisha safu ya kiungo, huku akimwona Anderson kama mrithi sahihi wa Kevin De Bruyne.

Adam Wharton

LICHA ya tetesi za Manchester United kutaka kumsajil kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton, klabu yake imesisitiza haina presha kuhusu mustakabali wake. Wharton, mwenye umri wa miaka 21, amekuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Palace. Kwa mujibu wa Sky Sports, Palace inaamini mchezaji huyo hajaomba kuondoka na atafanya hivyo ikiwa tu timu yake itakuwa tayari kumuuza.

Mateo Retegui

RIPOTI kutoka tovuti ya Fichajes zinadai Manchester United inapanga kumsajili mshambuliaji wa Al-Qadsiah, Mateo Retegui, raia wa Italia mwenye umri wa miaka 26. Inaelezwa Man United ipo tayari kulipa Pauni 52 milioni kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kuipata saini yake.

Retegui, aliyewahi kung’ara akiwa na Torino na Genoa, amekuwa na kiwango bora huko Saudi Arabia na msimu uliopita alicheza mechi 49 za michuano na kufunga mabao 28.

Kenan Yildiz

MSHAMBULIAJI wa Juventus na timu ya taifa ya Uturuki, Kenan Yildiz, 20, ameendelea kusisitiza hana mpango wa kuondoka katika timu hiyo na badala yake ameomba aongezwe mkataba licha ya kuwindwa na vigogo mbalimbali. Hadi sasa hakuna mwafaka uliofikiwa na mazungumzo baina ya wawakilishi wake na vigogo wa timu hiyo bado yanaendelea. Katika mkataba huo mpya Yildiz anahitaji takribani mara mbili ya mshahara wake.

Bradley Barcola

PARIS Saint-Germain inafanya mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya na mshambuliaji wao wa kimataifa wa Ufaransa, Bradley Barcola, 23, baada ya mchezaji huyo wa Ufaransa kuanza kuwindwa na timu mbalimbali kubwa za Ulaya ikiwemo Liverpool na Bayern Munich. Kwa mujibu wa tovuti ya L’Équipe, PSG inataka kumsainisha mkataba mpya Barcola kwa sababu pia amekuwa mmoja kati ya wachezaji wao tegemeo katika kikosi cha kwanza.

Dayot Upamecano

BARCELONA na Real Madrid zinatarajiwa kupambana vikali ili kumsajili beki wa kati wa Bayern Munich, Dayot Upamecano, 26, ambaye atakuwa mchezaji huru dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Man United pia inavutiwa na nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa, ambaye ana uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa. Upamecano, aliyesajiliwa na Bayern kutoka Leipzig kwa Euro 42 milioni mwaka 2021, amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya timu hiyo tangu wakati huo.

Joshua Zirkzee

AS Roma inatajwa kuwa kinara katika vita ya kuiwania saini ya  mshambuliaji wa Manchester United, Joshua Zirkzee, 24, dirisha lijalo.

Mabosi wa Roma wanahitaji kumsajili Zirkzee kwa mkopo wa nusu msimu ambao utakuwa na kipengele cha kumnunua mazima. Mbali ya Roma, staa huyu pia anawindwa na Como ya huko huko Italia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *