Chaumma ndicho chama kinachohesabika kubeba matumaini ya upinzani kwenye mbio za urais lakini mikutano yake ya kampeni imeshindwa kuvuta umati mkubwa wa watu.

    • Author, Na Charles William
    • Nafasi, Mchambuzi wa siasa Tanzania

Zimesalia wiki mbili pekee kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania kufanyika Oktoba 29, 2025. Tangu uliporejeshwa mfumo wa uchaguzi wa vyama vingi hapa nchini 1995, huu utakua uchaguzi mkuu wa kwanza utakaofanyika bila chama kikuu cha upinzani kushiriki, ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesusia kikishinikiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

Mzani wa kisiasa unaonekana kuegemea upande mmoja zaidi, kwani licha ya uchaguzi huu kuwa na wagombea urais kutoka vyama 17 ambao ni wengi zaidi ukilinganisha na uchaguzi wa 2005, 2010, 2015 na 2020 lakini shamrashamra za wagombea hapa nchini zimetawaliwa zaidi na mgombea wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati chama tawala hapa nchini CCM, kikiendelea na kampeni zake kwa kasi kikitumia mabasi makubwa zaidi ya 10, makumi ya magari binafsi kama Landcruiser ambayo yapo kwenye kila mkoa na wilaya, maelfu ya pikipiki ambazo zipo kwenye kila kata na maefu ya baiskeli za chama hicho ambazo zipo kwenye mitaa na vijiji, hali ni tete sana kwa vyama vya upinzani vinavyoshiriki uchaguzi.

Wagombea urais wengi wa upinzani wanatembea wakiwa na msafara wa gari mbili mpaka tatu pekee, huku gari moja likiwa ni lile walilosaidiwa kupewa na Tume ya Uchaguzi kama sehemu ya maombi yao ya kuwezeshwa ili washiriki uchaguzi huu kikamilifu. Huku wagombea ubunge wa upinzani wengi wao wakiwa hawana hata gari moja ya kuwawezesha kuzunguka kufikia wananchi.

Wagombea urais wa upinzani wengi wao wanalazimika kuhutubia wakiwa wamepanda juu ya magari yao katika mikutano mingi ili kukwepa gharama za kufunga majukwaa na kukodi vyombo vikubwa vya muziki. Pia kutokana na kutokua na fedha za kufanya matangazo ili kuhamasisha watu wajitokeze katika mikutano yao basi wanalazimika kuhutubia maeneo ya mikusanyiko kama sokoni na vituo vya mabasi.

.

Chanzo cha picha, CCM

.

Chanzo cha picha, ACT

Ingawa kuwa jumla ya wagombea urais 17 katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu lakini iwapo utakatiza barabarani katikati ya majiji makubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Arusha utakutana na mabango makubwa ya kampeni ya mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan kila unapotembea mita 200 au 300, lakini unaweza kuzunguka kwenye barabara za majiji hayo siku nzima bila kuona bango la mgombea urais wa chama cha upinzani.

Ili kuvutia maelfu ya wananchi kujitokeza kwenye mikutano yao, wagombea wa CCM wanatumia wasanii wa muziki wanaopendwa hapa nchini, ambao hulipwa mamilioni ya fedha ili kutumbuiza katika mikutano yao. Mathalani katika mikutano ya mgombea urais wa CCM kila mkutano umekua na wasanii wasiopungua 10 wanaotumbuiza kwa nyakati tofauti.

Wagombea ubunge wengi wa CCM katika kampeni zao wamekua wakiwalipa mamilioni ya fedha wasanii wa muziki ili waende kutumuiza na kuvutia wananchi. Wasanii maarufu hapa nchini kama Harmonize, Mbosso na Zuchu ambao hutoza kiwango cha malipo cha shilingi milioni 20 mpaka milioni 40 kwa onesho moja wamekua na mfululilizo wa ratiba za kutumbuiza kwenye kampeni za CCM.

Matumaini ya ACT ya kusimamisha mgombea urais yamezama mahakamani na hivyo chama hicho kimeshindwa kufanya kampeni kubwa za kitaifa.

Chanzo cha picha, ACT

Mgombea ubunge wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) John Lema amenieleza kuwa kama angepata angalau shilingi milioni 30 au 40 angeweza kufanya kampeni zake kwa ufanisi lakini kutokana na kutokua na fedha analazimika kufanya kampeni za kutembea mguu mtaa kwa mtaa na katika nyumba za watu kuomba kura.

Kiwango cha fedha anachotamani kukipata mgombea huyu ili afanye kampeni kwa ufanisi ni kiwango kidogo sana ambacho wagombea ubunge wa CCM katika maeneo mbalimbali nchini wanakitumia kumlipa msanii mmoja tu wa daraja la juu kama kama Marioo, Harmonize, Mbosso au Zuchu kwa onesho moja tu analofanya katika mikutano ya chama hicho.

Jimbo la Arusha Mjini lina mitaa 154 ambayo mgombea anatakiwa kuifikia kuomba kura, lakini siku ya uchaguzi litakuwa na jumla ya vituo 1053 vya kupigia kura ambavyo mgombea na chama chake watalazimika kuweka mawakala zaidi ya elfu moja ili kuhesabu kura. Mawakala hao ni lazima walipwe posho za kufanya kazi hiyo, wapelekewa chakula cha mchana lakini pia lazima wakusanywe na kupewa mafunzo kabla ya uchaguzi.

Nilijaribu kumdodosa Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Benson Kigaila kuhusu hali mbaya ya kifedha ya wagombea ubunge wa chama chake kiasi cha wengi wao kushindwa hata kufanya mikutano ya hadhara, akaniambia chama hicho kilitarajia kupata fedha kutokana na michango mbalimbali ya wadau lakini hali imekua ngumu tofauti na walivyotarajia.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Haruna Lipumba ambaye pia amewahi kugombea urais wa Tanzania mara tano (mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2020), lakini mwaka huu ameamua kupumzika yeye aliniambia ili kuratibu na kukamilisha kampeni za mgombea urais wa chama hicho kwa ufanisi inahitajika angalau kiasi cha shilingi milioni 600 ambacho ni ngumu kwao kuzipata.

Serikali ya Tanzania imekua ikilipa fedha za ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa vyama vya siasa hapa nchini, lakini fedha hizo hutolewa kulingana na asilimia za kura za wagombea ubunge wa chama husika katika uchaguzi uliopita. Kutokana na matokeo mabaya ya vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita vyama hivyo vinapata fedha kiduchu sana.

Wakati CCM ikipata zaidi ya shilingi bilioni moja kila mwezi, chama kikuu cha upinzani CHADEMA ambacho kiligomea kushiriki uchaguzi wa mwaka huu kikishinikiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi chenyewe kinapata shilioni milioni 107 kwa mwezi, huku chama cha ACT Wazalendo chenyewe kikipata milioni 10 tu kwa mwezi na CUF kikipata shilingi milioni 8.5 tu kwa mwezi.

Maneno mengi hakuna wagombea wa upinzani kabisa

Hata hivyo udhaifu mkubwa wa upinzani mwaka huu haupo kwenye kutokua na fedha za kufanyia kampeni tu, bali hali ni tete hata kwenye kupata wagombea wa nafasi mbalimbali kwani katika majimbo zaidi ya 100 kati ya 272 havina wagombea ubunge, lakini pia havina wagombea udiwani katika kata zaidi ya elfu moja, kati ya kata 3960.

Katika mkoa wa Dodoma, yalipo makao makuu ya serikali vyama vya upinzani wamefanikiwa kusimamisha wagombea ubunge katika majimbo yote 11 hata hivyo kwenye nafasi za udiwani wameshindwa kusimamisha wagombea katika kata 114 kati ya 206. Kwa takwimu hizi maana yake asilimia 55 ya kata za mkoa huo hazina wagombea kutoka vyama vya upinzani.

Hali ni mbaya zaidi katika mkoa wa Geita ambako vyama vya upinzani vimeshindwa kusimamisha wagombea katika majimbo 8 kati ya 9, hivyo lakini pia wameshindwa kupata wagombea udiwani katika kata 100 kati ya 122. Maana yake katika mkoa huo asilimia 83 ya kata zina wagombea udiwani wa CCM pekee.

Katika mkoa wa Ruvuma, Kusini mwa Tanzania upinzani umeshindwa kupata wagombea ubunge katika majimbo mawili kati ya tisa lakini umeshindwa kusimamisha wagombea udiwani katika 50% ya kata kwani kuna wagombea udiwani wa upinzani kata 87 tu kati ya 173 za mkoa huo. Mkoa wa Tabora, Magharibi mwa Tanzania upinzani umeshindwa kusimamisha wagombea udiwani kata 112 kati ya 203 sawa na 56%

Hali ya kutokuwepo kwa wagombea ubunge na udiwani katika majimbo na kata nyingi imetawala sana, hivyo katika maeneo hayo wananchi watapiga kura za “Ndiyo” au “Hapana” kwa mgombea mmoja pekee wa chama tawala ambaye jina na picha yake itakuwepo katika karatasi za kupigia kura.

Kutokana na kutokuwepo kwa wagombea imara wa upinzani katika kata na majimbo mengi, hivyo wagombea ubunge wengi wa CCM wamekua wakipata mapumziko ya kutosha katika kipindi hiki cha kampeni, tofauti na miaka iliyopita ambapo wagombea hao walikuwa wakilazimika kufanya kampeni siku zote 60 za kampeni au kupumzika siku zisizozidi tano tu.

Baadhi ya wagombea ubunge wa CCM wanaondoka kwenye majimbo yao kwa wiki mbili mpaka tatu na kuzunguka na msafara wa mgombea urais katika mikoa mbalimbali au Kwenda katika majimbo mengine kunadi wagombea jambo ambalo lilikua si rahisi kuliona katika miaka mingine ya uchaguzi kutokana na fukuto kali lililokuwepo kwenye kata na majimbo yao.

Dalili za chama tawala kupata ushindi mkubwa pengine kuliko ushindi wowote ambao kimewahi kupata katika siasa za vyama vingi zinaonekana waziwazi. Mtihani mkubwa pekee unaobaki kwa CCM ni kuhamasisha wapiga kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura, kwani lipo kundi kubwa la wananchi wanaoamini kauli mbiu ya “NO REFORMS, NO ELECTION” inayosimamiwa chama kikuu cha upinzani – CHADEMA kinachopinga uchaguzi kufanyika.

*Makala hii ni uchambuzi na maoni binafsi ya mwandishi na si msimamo wa BBC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *