Makumi ya miji na mikoa kote Uhispania imeshuhudia maandamano makubwa na migomo ya umma ya mshikamano na watu wa Gaza . Migomo na maandamano hayo makubwa ya nchi nzima yalifanya jana Jumatano.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa maandamano hayo yalifanyika katika miji na mikoa takriban 200, na washiriki wakiwa wameshikilia bendera na mabango ya Palestina yenye nara kama vile “Uhuru wa Gaza,” “Komesha mzingiro,” na “Hapana kwa vita, ndio kwa haki,” walitaka kukomeshwa kabisa kwa vikwazo na kuondolewa kikamilifu mzingiro dhidi ya Gaza na kutekelezwa kikamilifu vipengee vya makubaliano ya kusitisha vita.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Pedro Sanchez Waziri Mkuu wa Uhispania amesisitiza kuwa, makubaliano ya kusitisha vita Gaza yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Israel yasifanywe kuwa fidia ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Israel Ukanda wa Gaza.

Mwezi Novemba mwaka jana Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa waranti wa kutiwa mbaroni Netanyahu na Yoav Gallant Waziri wa zamani wa Vita wa Israel kwa kutekeleza jinai za kivita dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. 

Uhispania ambayo ni miongoni mwa nchi wakosoaji wakubwa wa mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza Septemba mwaka huu ilitangaza kuwa mwendesha mashtaka wa nchi hiyo kwa kushirikiana na mahakama ya ICC atachunguza “ukiukwaji mkubwa” wa haki za binadamu uliofanywa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa uratibu na ICC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *