
Umoja wa Afrika umechukua hatua haraka kufuatia hatua ya jeshi kuchukuwa madaraka nchini Madagascar. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, Oktoba 15, Umoja wa Afrika umeisitisha Madagascar kwenye taasisi zake mara moja. Nchi nyingine kadhaa katika bara hilo pia zimesitishwa kwenye taasisi na shughuli za AU kufuatia mapinduzi ya kijeshi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika linalaani vikali hatua ya jeshi kuchukuwa madaraka nchini Madagascar na linafutilia mbali kabisa mabadiliko hayo kinyume na katiba, ambayo yanakiuka kanuni za AU, kwa mujibu wa taarifa yake. Kwa hivyo nchi hii imesitishwa kwenye taasisi na shughuli zake mara moja hadi utaratibu wa kikatiba urejeshwe.
Katika taarifa yake, Baraza la Amani na Usalama pia linavitaka vikosi vya jeshi vya Madagascar kuacha kuingilia masuala ya kisiasa, la sivyo vikwazo vinaweza kuwekwa dhidi ya wale waliohusika katika mapinduzi ya kijeshi. linatoa wito wa kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba kupitia serikali ya mpito ya kiraia na kwa ajili ya kuandaa uchaguzi haraka iwezekanavyo, pamoja na kufanyika kwa mazungumzo jumuishi ya kitaifa.
Hatimaye, taarifa hiyo inakaribisha uamuzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kutuma wajumbe katika Kisiwa hiki na inapendekeza AU kufanya vivyo hivyo. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, SADC ilisema “imesikitishwa” na ripoti za jaribio la “mapinduzi” nchini Madagascar. Ujumbe huo, ambao lengo lake ni “kuwezesha kurejea kwa haraka kwa utaratibu wa kikatiba,” utaongozwa na Dk. Joyce Banda, Rais wa zamani wa Malawi.