
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza leo kuwa zaidi ya watoto 650,000 Wapalestina wanakosa elimu katika Ukanda wa Ghaza kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Katika taarifa iliyoweka kwenye mtandao wa X, UNRWA imesema: “huko Ghaza, watoto hawako maskulini kwa mwaka wa tatu mfululizo. Kwa wasichana na wavulana wapatao 660,000, kurudi masomoni hakuhusu elimu tu, lakini kunahusu pia kuanza kupona kuondokana na kiwewe kikubwa.”
Taarifa ya UNRWA imeendelea kueleza kwamba, likiwa ndilo shirika kubwa zaidi la misaada ya kibinadamu huko Ghaza, liko tayari kutoa msaada na uungaji mkono kwa watoto hao.
Tamara Alrifai, mkurugenzi wa UNRWA anayehusika na mahusiano ya nje, amesema, “kipaumbele kwa UNRWA ni elimu kwa watoto na kuanza tena watoto kupata masomo”.
Tangu Oktoba 2023, vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel yameshawaua shahidi karibu Wapalestina 68,000 katika Ukanda wa Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuifanya sehemu kubwa zaidi ya eneo hilo iwe haiwezi kukalika.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), mashambulizi hayo ya jeshi la kizayuni yameteketeza kwa kiwango fulani au kikamilifu 97% ya majengo ya skuli za Ghaza.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa kati ya utawala wa kizayuni wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS wiki iliyopita, kulingana na mpango uliowasilishwa na Rais wa Marekani Donald Trump. Awamu ya kwanza ya mpango huo inajumuisha kuachiliwa huru mateka wa Israel mkabala wa kuachiwa huru Wapalestina waliokuwa wakiteseka kwenye magereza ya utawala huo ghasibu…/