Simanjiro. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Losoito wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wataondokana na adha ya msongamano kwenye madarasa baada ya wadau wa elimu kuwajengea madarasa mengine mawili.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2003 hivi sasa ina wanafunzi 634 na vyumba saba vya madarasa.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Losoito, wakizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 16, 2025, wamelishukuru Shirika lisilo la kiserikali la Ako Tanzania Community Support kwa kuwajengea madarasa mawili katika shule hiyo.

Mkazi wa kijiji cha Losoito, Tipiliti Kuya amesema shirika hilo limewajengea darasa la awali na sasa wanajenga madarasa mengine mawili mapya.

“Awali watoto walikuwa wanasomea chini ya miti na kugaragara kwenye udongo ila kwa msaada huu wa Ako wa ujenzi wa madarasa hayo watasoma katika mazingira mazuri,” amesema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Loishiye Laizer amelishukuru shirika hilo kwa kusaidia kuongeza ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.

Laizer amesema jitihada za Ako zimeonekana kwani walikuwa na wakati mgumu ila waliwapatia vifaa vya kufundishia wanafunzi wa shule ya awali.

“Tulikuwa na wakati mgumu ila Ako wametujengea madarasa hayo, pia wametupatia madawati 20 meza ya walimu na viti, kwa kweli wameiunga mkono serikali katika kusaidia jamii,” amesema mwalimu Laizer.

Mwenyekiti wa kijiji cha Losoito, Samson Sakwei ameeleza kuwa shirika hilo limekuwa msaada kwao kwani maendeleo waliyofanya katika sekta mbalimbali ni makubwa mno.

Sakwei ameeleza kuwa pamoja na elimu, wamemalizia zahanati ya kijiji na choo cha kisasa na kufanikisha mradi wa lishe wa kikundi cha wanawake wa kilimo cha mbogamboga.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Hilda Kimathi amesema kuwa wamesaidia jamii ya eneo hilo kwa kujenga madarasa, kumalizia zahanati na kuwezesha vikundi vya wanawake wanaolima mbogamboga.

Kimathi amesema walipokea ombi toka Losoito na wakajenga darasa la awali na sasa wanajenga madarasa mengine mawili ambayo yatazinduliwa hivi karibuni yakikamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *