Musoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amewahimiza walimu nchini wasichoke kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya dunia yanayoendelea kutokea katika nyanja mbalimbali za elimu na teknolojia.

Akizungumza leo Alhamisi, Oktoba 16, 2025, katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara wakati akifungua semina ya viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Kanda ya Ziwa na Ziwa Magharibi, iliyowakutanisha viongozi kutoka mikoa minane, Dk Biteko amesema Serikali itaendelea kuboresha maisha ya watumishi wake, wakiwamo walimu kwa kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa wakati.

“Rais wa CWT amesema hapa kuwa viongozi wote ni wapya, hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa ufanisi na ubunifu kwa kuzingatia kuwa dunia imebadilika. Mimi ni zao la mwalimu na nimehudumu kwenye taaluma hii. Tulikuwa tukidai mambo haya haya, mishahara, posho za kufundishia na nauli, Serikali imefanya mengi kuboresha hali za walimu huku ikiendelea kutafuta suluhisho kwa changamoto zilizobaki,” amesema Dk Biteko.

Ameongeza kuwa ni vyema walimu wakatambua na kuthamini hatua nzuri zilizopigwa na Serikali, huku wakiendelea kudai haki zao kwa njia ya staha na kujenga.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu imeendelea kuboresha miundombinu ya shule na rasilimali za kufanikisha miradi ya elimu nchini.

Aidha, amebainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutoa ajira zaidi za walimu 7,000 wa masomo ya Hisabati na Sayansi ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Hivyo, ametoa rai kwa walimu kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, ili kuwachagua viongozi wanaoamini wataendeleza maendeleo ya taifa.

“Hakuna nchi inayoweza kupata viongozi wa kidemokrasia bila wananchi kujitokeza kupiga kura. Hivyo nawakumbusha walimu kutumia haki yenu ya kikatiba kuchagua viongozi bora, jambo ambalo litawapa uhalali wa kudai maendeleo,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amesema Serikali ya CCM inayoongozwa na Samia imefanya maboresho makubwa katika kada ya ualimu, ikiwamo kuboresha maslahi na mazingira ya kazi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akisalimiana na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CWT anayewakilisha Walimu wenye ulemavu Taifa, baada ya kufungua Semina ya Viongozi wa CWT Kanda ya Ziwa Victoria na Kanda ya Magharibi Iliyofanyika Oktoba 16, 2025 wilayani Musoma Mkoa wa Mara.

Naye Rais wa CWT Taifa, Dk Suleiman Ikomba ameipongeza Serikali kwa jitihada hizo na kuiomba iendelee kukiona chama hicho kama mshirika muhimu katika kuinua taaluma ya elimu nchini.

Amesema CWT inaamini demokrasia ni chachu ya maendeleo, hivyo chama kimejipanga kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Katika risala yao, viongozi wa CWT wameiomba Serikali kuangalia upya suala la posho za kufundishia na nauli, pamoja na kulipa madeni ya likizo, uhamisho na stahiki za wakuu wa idara.

Pia, wamemshukuru Rais Samia kwa nyongeza ya mishahara, kupandishwa vyeo, madaraja na hatua za kulipa madeni ya walimu zilizokuwa zimesalia kwa muda mrefu.

Semina hiyo yenye kaulimbiu Uchaguzi Mkuu ni Jukumu Letu: Walimu Kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025imehusisha zaidi ya walimu 470 kutoka mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kigoma, Tabora na Kagera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *