Dar es Salaam. Wasanii wa Filamu na Muziki wamekuwa wakifuatiliwa na wengi katika mitandao ya kijamii hasa Instagram kutokana na umashuhuri wa kazi zao. Pia watoto wao ambao wameamua kuwaweka kwenye mtandao huo nao wamejizolea umaarufu wa kiasi chake.

Makala haya yanaenda kuangazia watoto 10 wa Mastaa kutokea Bongo ambao wamejizolea wafuasi (Followes) wengi kwenye mtandao wa Instagram. Data hizi zimetoka kwenye kurasa rasmi ambazo zinasimamiwa na wazazi wao.

1. Tiffah wa Diamond na Zari

Tiffah alizaliwa August 6, 2015 na kuwa mtoto maarufu zaidi Bongo, hii ni kutokana na nguvu ya ushawishi waliyonayo wazazi wake (Diamond na Zari) hasa ukanda wa Afrika Mashariki.

Novemba 2016 alikuwa mtoto wa kwanza Tanzania kuweza kufikisha Followers Milioni 1 kwenye ukurasa wake wa Instagram. Hadi kufikia sasa ndiye anaongoza kwenye mtandao huo akiwa anafuatiliwa na watu zaidi ya Milioni 4.6.

2. Nillan wa Diamond na Zari

Mtoto huyu wa pili kwa Diamond na Zari alizaliwa December 6, 2017  kwenye hospitali ya Netcar ya Pretoria nchini Afrika Kusini, alikuwa na umaarufu wake kiasi lakini hakuweza kufikia kiwango cha ule wa dada yake, Tiffa.

Kwa sasa anafuatiliwa na watu zaidi ya Milioni 1.8 kwenye ukurasa wake wa Instagram, akiwa amempiku Jaydan wa Rayvanny na Fahyvanny.

3. Naya wa Billnass na Nandy

Kenaya maarufu ‘Naya’ alizaliwa Agosti 17, 2022 ni miongoni mwa watoto wa mastaa wanaofanya vizuri katika kiwanda cha muziki licha ya kuwa na miaka mitatu tu lakini mtoto huyo amekuwa akifuatiliwa sana katika mitandao ya kijamii huku mashabiki wengi wakivutiwa zaidi na upole wake.

Hadi kufikia sasa Naya anafuatiliwa na zaidi ya watu 774,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram sehemu pekee ambayo wazazi wa mtoto huyo wanaitumia kushare matukio yake akiwa nyumbani pamoja na shuleni.

4. Jaydan wa Rayvanny na Fahyvanny

Jaydan alizaliwa Aprili 15, 2017 na amekuwa miongoni mwa watoto wa Mastaa wenye umaarufu sana, Baba yake katika muziki ni mshindi wa Tuzo ya BET, Mama yake pia ni mshindi wa Tuzo ya Best Dressed Lady kutoka Starqt Awards nchini Afrika Kusini.

Hadi kufikia sasa anafuatiliwa na watu zaidi ya 357,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram, hivi majuzi alipata Tuzo kutokea East Africa Fashion Awards, hivyo ni familia ya Tuzo tu.

5. Jaden wa Ray Kigosi na Chuchu Hansy

Alizaliwa January 8, 2017 wazazi wake ni wasanii wenye nguvu kubwa sana ushawishi kwenye kiwanda cha filamu Bongo. Jaden naye ni maarufu mtandaoni kwa kiasi chake hadi kupata nafasi ya kuwa balozi wa moja ya maduka makubwa ya kuuza nguo jijini Dar es Salaam.

Hadi kufikia sasa anafuatiliwa na watu zaidi ya 265,000 kwenye ukurasa wake ambao ndio kama uwanja wa kuuza bidhaa ambazo amepatiwa na kampuni mbalimbali akiwa kama Balozi wao.

6. Sasha wa Sugu ‘Mr. II’ na Faiza Ally

Alizaliwa September 25, 2012, Baba yake ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo kabisa kukuza muziki wa Hip Hop Bongo kabla ya kuingia kwenye siasa, Mama yake ni amejikita zaidi kwenye filamu na biashara.

Wanaomfuatilia mtoto Sasha ni zaidi ya 265, 000 kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mama yake anajitahidi sana kuweka kila kitu kinachomuhusu Sasha kwenye ukurasa huu kwa wakati tofauti na Mastaa wengine. Huku akikadiriwa kuongeza wafuasi zaidi siku zijazo kutokana na matangazo ya mavazi anayoyafanya.

7. Naseeb Junior wa Diamond na Tanasha

Naseeb Junior alizaliwa October 2, 2019 akiwa ni mtoto wa tatu wa kiume kwa Diamond, kwa sasa anaishi na mama yake nchini Kenya ambapo anafanya muziki.

Zaidi ya watu 443,000 wanamfuatilia kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram ingawa kumekuwa na kurasa nyingi zinazofuatiliwa na wengi ila hazipo katika mikono ya wazazi wake.

8. Fantasy wa Majizzo na Hamisa Mobetto

Mtoto Fantasy alizaliwa April 10, 2015, wazazi wake walimficha kwa kipindi cha miezi sita hadi October 10, 2015 ambapo ndipo picha zake ziliweza kuonekana mtandaoni tofauti na watoto Mastaa wengine ambao huonyeshwa baada ya kumalizika 40.

Fantasy hadi sasa anafuatiliwa na watu zaidi 249,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao unasimamiwa na mama yake. Pia mdogo wake, Dylan ambaye ni mtoto wa Diamond na Hamisa anafuatiliwa na watu zaidi 49,000 katika ukurasa wake rasmi.

9. Kiba Junior wa Alikiba

Mtoto Kiba Junior husherekea siku yake ya kuzaliwa kila ifikapo June 20, wadogo zake, Nutayla na Keyaan nao pia wapo katika mtandao huo pendwa.

Watu zaidi ya 189,000 wanamfuatilia kwenye ukurasa wake wa Instagram, miaka takribani mitatu iliyopita alikuwa amezidiwa idadi ya wanaomfutilia na dada yake, Amiya Kiba ila kwa sasa kamzidi.

10. Amara wa Marioo na Paula Kajala

Amara amezaliwa Mei 3,2024 akiwa na mwaka mmoja tuu mtoto huyo ameonesha kuwa tishio kwa baadhi ya watoto wa mastaa kutokana na kufuatiliwa zaidi katika mtandao wa Instagram.

Mpaka kufikia sasa anafuatiliwa na watu 284,000 katika Instagram yake huku video zake baadhi zikipata watazamaji zaidi ya milioni moja.

Mbali na Amara mtoto mwingine wa staa anayekuja kwa kasi ni Price Rakeem wa Jux na Priscilla ambaye ndani ya miezi mitatu anawafuasi 219,000 katika ukurasa wake wa Instagram.

Mtoto huyo ameiteka mitandao ya kijamii mama yake Pricy ni mwigizaji nguli kutoka Nigeria baba yake ni msanii anayetikisa zaidi katika muziki wa Bongo Fleva.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *