
Zaidi ya watalii milioni 3.5 wa kigeni wameitembelea Iran katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, Waziri wa Turathi za Utamaduni, Utalii na Sanaa, Reza Salehi Amiri alisema hayo jana Jumatano.
Amesema idadi ya watalii waliokuja hapa nchini katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka huu ilipanda kwa wastani wa 30% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana,
Hata hivyo amebainisha kuwa, watalii walioingia hapa nchini walipungua katika miezi mitatu iliyofuata kutokana na vita vya siku 12 vya kutwishwa na Israel.
“Idadi ya watalii wanaowasili nchini ilirejea katika viwango vya kawaida katika miezi iliyofuata,” Waziri Amiri amesema na kuongeza kuwa, idadi ya watalii wa kigeni wanaokuja hapa nchini imeongezeka licha ya matukio ya kisiasa na kijeshi yanayoshuhudiwa sasa katika eneo la Asia Magharibi.
Kufuatia kuongezeka idadi ya watalii, sekta ya ajira nayo pia imeweza kustawi nchini Iran. Waziri wa Utalii wa Iran amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalenga kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea nchi hii hadi milioni 15 kwa mwaka.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi yenye ustaarabu mkongwe na hivyo ina vivutio vingi vya kitalii kwa wapendao historia.
Aidha Iran ina vivutio vingi ya Kiislamu hasa maeneo ya ziara ambayo hutumbelewa na Waislamu kama vile Haram Takatifu ya Imam Ridha AS mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran na Haram Takatifu ya Bibi Maasuma SA katika mji wa Qum kusini mwa Tehran.