Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imebaini kuwa moja kati ya maambukizi sita ya bakteria yaliyothibitishwa na maabara duniani mwaka 2023 yalionyesha usugu dhidi ya dawa za antibiotiki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya mwaka 2018 na 2023, usugu wa antibiotiki umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 kwa bakteria na antibiotiki zilizofuatiliwa, likiwa ongezeko la wastani wa kati ya asilimia tano hadi 15 kila mwaka.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, amesema Serikali inafuatilia kwa karibu taarifa hiyo ya WHO na itatoka na mikakati madhubuti ya kupunguza tatizo hilo, ambalo pia limeanza kushika kasi nchini.

Ameeleza kuwa utafiti wa mwisho uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2019 ulionyesha matumizi ya dawa dhidi ya vimelea nchini yalifikia asilimia 62.3, sambamba na makadirio ya usugu wa antibiotiki kwa asilimia 59.8, huku wengi wakibainika kutumia dawa hizo bila ushauri wa daktari.

Kuhusu ripoti

Takwimu zilizoripotiwa kwa Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi na Usugu wa Antibiotiki wa WHO (GLASS) kutoka zaidi ya nchi 100, zinaonya kuwa ongezeko la usugu wa antibiotiki muhimu ni tishio linalokua kwa afya ya dunia.

Ripoti hiyo mpya ya mwaka 2025 inatoa kwa mara ya kwanza makadirio ya kiwango cha usugu katika aina 22 za antibotiki zinazotumika kutibu maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), njia ya chakula, damu na magonjwa ya kisonono.

WHO inasema ripoti hiyo inahusu aina nane za bakteria wa kawaida, ambao kila mmoja anahusishwa na moja au zaidi ya maambukizi hayo, ikieleza pia kuwa usugu huo wa antibiotiki hutofautiana duniani kote.

Shirika hilo linakadiria kuwa usugu huo ni wa kiwango cha juu zaidi katika Kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia na Kanda ya Mediterania ya Mashariki, ambako moja kati ya maambukizi matatu yaliyoripotiwa yalikuwa na usugu.

“Katika Kanda ya Afrika, moja kati ya maambukizi matano yalikuwa sugu. Usugu pia ni wa kawaida na unaongezeka zaidi katika maeneo ambako mifumo ya afya haina uwezo wa kugundua au kutibu bakteria wanaosababisha maambukizi,” inaeleza ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba 13, 2025 Geneva, nchini Uswisi.

“Usugu wa antibiotiki unazidi maendeleo ya tiba za kisasa na unatishia afya ya familia duniani kote,” alisema Dk Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Amesema kwa kadri nchi zinavyoimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR), ni muhimu antibiotiki kutumika kwa uangalifu.

WHO imezitaka nchi zote kuripoti data zenye ubora wa juu kuhusu AMR na matumizi ya antibiotiki kwa GLASS ifikapo mwaka 2030.

Kupambana na usugu wa vimelea vya dawa, (AMR) ni miongoni mwa vipaumbele vya Mkurugenzi Mkuu WHO Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi.

Akinadi sera zake Mei, 2025 wakati akiwania nafasi hiyo ambayo aliishinda, alisema AMR ni tatizo linalosababisha vifo milioni 1.2 kila mwaka, huku asilimia 40 ya mataifa ya Afrika yakikosa takwimu za ufuatiliaji. Aliahidi kuanzisha hifadhi data za kikanda kukabiliana na tatizo hilo.

Maoni ya mfamasia

Akizungumza na Mwananchi, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah amesema ili kukabiliana na changamoto ya usugu wa antibiotiki sheria lazima ifuatwe ili afya isiwe biashara.

Amesema kwa sasa dawa ni chanzo cha fedha kwenye vituo vya afya, hivyo uangalizi uwepo na elimu kwa jamii itolewe ili antibiotiki zisitolewe kiholela.

Hezekiah amesema suala la usugu wa dawa hizo ni mtambuka, hivyo ni muhimu kuwapo ushirikiano wa sekta zingine zikiwamo za kilimo na ufugaji.

“Tuangalie dawa zinatumikaje kwenye kilimo au mifugo, kuna ongezeko la chembechembe za dawa kwenye mazingira yetu hili ni suala ambalo wataalamu wenzetu kwa pamoja tushirikiane,” ameshauri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *